Murray aondolewa na Nadal

Bingwa mtetezi wa mashindano ya Wimbledon yanayofanyika nchini Uingereza, Rafa Nadal amemshinda Muingereza Andy Murray na kuzima ndoto ya Waingereza kumpata bingwa Muingereza wa kwanza katika kipindi cha miaka 75.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Tumaini la Uingereza

Nadal amemshinda Murray kwa kipigo cha uhakika kwa seti tatu kwa moja baada ya Andy Murray kuwapa matumaini mashabiki wake waliofurika uwanja wa kati ya Wimbledon akiondoka na ushindi wa 7-5.

Baada ya seti hiyo Murray aliendelea hivyo hadi mchezo wa tatu Nadal alipoanza kutoa makucha yake na kubadili mchezo hatimaye akishinda 6-2, 6-2, 6-4.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rafael Nadal

Nadal ambaye hadi wakati huu alikuwa namba moja atapambana na Novak Djokovic ambaye alifuzu kwa fainali inayochezwa siku ya jumapili kumpata bingwa wa mwaka huu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Novak Djokovic
Haki miliki ya picha AP
Image caption Jo Wilfred Tsonga

Licha ya kushinda nusu fainali ya kwanza, Novak Djokovic kutoka Serbia alipewa kibarua na Mfaransa Jo-Wilfred Tsonga ambaye babake alitoka Jamhuri ya Congo. Andy Murray alijitahidi katika mchezo huu lakini maarifa na utayarifu wa Nadal ulimzidi na kudhihirisha tofauti baina ya mwanafunzi na mwalimu.

Nadal ambaye wiki ijayo atapoteza nafasi yake ya kuwa mchezaji bora duniani kwa Novak Djokovic ameonyesha nia ya moyo wa kutaka kushinda mashindano haya tangu mwanzo.

Djokovic atatangazwa mchezaji namba moja duniani wiki ijayo kutokana na kufululiza kushinda mashindano mengi aliyoshiriki mwaka huu.