Baada ya kipigo: David Haye itakuwaje?

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Haye alipokea kipigo

Bondia David Haye ameambia BBC kuwa atafanya uamuzi juu ya mustakabali wake katika ndondi "wiki chache zijazo" baada ya kushindwa na Wladimir Klitschko katika pambano la uzani wa juu siku ya Jumamosi.

''Nimejipa muda wa miezi mitatu , katika mchezo wa ndondi huu si muda mrefu," raia huyo wa Uingereza amemwambia mwandishi wa BBC Olly Foster.

Hata hivyo,bondia huyo mwenye umri wa miaka 30 pia alisema angependa "pambano la marudiano" na Klitschko.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Vitaly Klitschko alimkung'uta David Haye

Haye alipambana katika raundi zote 12 kabla ya majaji kuamua kuwa ameshindwa kwa wingi wa pointi ikiwa ni 117-109, 118-108 na 116-110 na kumpa ushindi raia wa Ukraine mwenye umri wa miaka 35 Klitschko.

Haye alimpongeza Klitschko, akisema "ni bondia hodari",lakini alisema tatizo la yeye kutoonyesha uhodari wake ni kutokana na kuumia kidole cha mguu.

Pia alisema kuna mambo mengine ambayo yalimtatiza katika ukumbi wa Hamburg Imtech.

"Kulikuwa na hila nyingi," aliongeza Haye,ambaye alipoteza taji lake la WBA kwa bingwa wa IBF na WBO Klitschko.

"Tulikuwa na muamuzi ambaye hakuchukua hatua kwa makosa aliyofanya Klitschko. Kulikuwa na mambo madogo madogo yanafanyika huko nyuma.

"Lakini nikafkiri,hata kama muamuzi haoni baadhi ya mambo ningepata njia ya kushinda kwa vyovyote.Lakini usiku huo alikuwa bora zaidi yangu."