Mo Farah atimka katika mbio za mita 5,000 katika mashindano ya dunia ya riadha, Daegu, Korea Kusini, na kujinyakulia medali ya dhahabu.

Mo Farah Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mo Farah amepata medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia mita 5,000

Mwanariadha wa Uingereza, Mo Farah alitimka kadri ya uwezo wake wote katika mbio za mita 5,000, mashindano ya riadha ya dunia, mjini Daegu, Korea Kusini, na hatimaye kujinyakulia medali ya dhahabu katika mashindano hayo.

Farah, wiki iliyopita, alifanikiwa kupata medali ya fedha katika mbio za mita 10,000.

Farah alisubiri hadi mita 400 za mwisho kabla ya kwenda kwa kasi zaidi hatua iliyosalia, akitumia sekunde 52.87, na hatimaye kumaliza katika nafasi ya kwanza kwa muda wa dakika 13, sekunde 23:37.

Alionekana kuachwa nyuma katika mita 2,000 za kwanza, akiwa katika kundi kubwa la wanariadha, lakini hatua za mwisho aliongeza kasi na kujihakikishia dhahabu.

Mmarekani Bernard Lagat, alichukua medali ya fedha, huku Imane Merga wa Ethiopia akimaliza mbio hizo katika nafasi ya tatu.