Paul Ince ameishambulia timu ya taifa ya soka ya England, akidai kwamba wachezaji wengi hawatambui ni jambo la fahari kuichezea nchi yako

Paul Ince Haki miliki ya picha Getty
Image caption Amewalaumu wachezaji wa timu ya taifa ya England kwa kutocheza kwa moyo wao wote

Ince alikuwa akizungumza katika matangazo ya BBC ya Radio 5 Live.

"Kuichezea England ilikuwa ni kufikia kilele cha mchezo wako. Sasa sio muhimu sana kwa kuwa kuna ligi ya klabu bingwa na ligi kuu ya Premier", alifafanua Ince.

Matamshi ya nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England ni kufuatia England kuponyoka kwa ushindi finyu wa 1-0 dhidi ya Wales katika uwanja wa Wembley, Jumanne iliyopita.

Ince, ambaye wakati mmoja aliichezea Manchester United ya England, na vile vile Inter Milan ya Italia, anasema wachezaji pia hutoa visingizio vingi wanapohitajika kuichezea timu ya taifa.

"Iwapo utaitwa kuiwakilisha nchi, ni lazima uhakikishe upo. Siku hizi, kuna watu wanaotoa vijisababu - wamechoka, au wamejeruhiwa - kwa sababu wanataka wawe katika hali nzuri ili waweze kushiriki katika mechi ya mwishoni mwa wiki".

"Nilipoichezea England, kulikuwa na wachezaji waliokuwa katika kikosi mwezi mzima, au katika kila mashindano, lakini (kutokana na ligi ya klabu bingwa na Premier) sasa tuna wachezaji 40 wanaopata kuichezea nchi na wasiostahili. Inasikitisha", alielezea Ince.

Ince pia aliwalaumu mashabiki wa England kwa kutoshangilia kikamilifu uwanjani wakati timu ilipocheza dhidi ya Wales, na akasema anaamini timu ya England huwa na wasiwasi inapocheza Wembley.