Gary Cook amesema alifanya uamuzi usiofaa katika kumuandikia barua pepe ya kejeli mamake Nedum Onuoha ambaye anaugua saratani

Meneja wa klabu tajiri ya Man City, Garry Cook, amejiuzulu kufuatia madai kwamba alimwandikia barua pepe Dr Anthonia Onuoha, mamake mlinzi wa klabu hiyo, Nedum Onuoha, akimfanyia kejeli kuhusu hali yake ya afya.

Image caption Akiri kuandika barua pepe isiyofaa

Dk Onuoha anaugua saratani.

Bodi ya Man City imesema imeipokea barua ya Cook kujiuzulu kwa masikitiko, naye Cook alikiri alifanya kosa la utendaji, kwa uamuzi usiofaa.

Cook alikubali kujiuzulu, baada ya klabu ya Man City kusema "kimsingi kuna ukweli fulani" katika madai hayo.

Awali alikuwa amekanusha kutuma ujumbe huo, akidai kwamba kuna watu waliofanikiwa kuingilia akaunti yake ya barua pepe.

Katika wavuti ya klabu, Man City imethibitisha kwamba imeikubali hatua hiyo ya Cook kujiuzulu, na mwenyekiti Khaldoon Al-Mubarak amemuomba msamaha Dk Onuoha.

Mamake mlinzi huyo wa Man City, huwa ni wakala wa mchezaji huyo.

Awali aliwatumia barua pepe Marwood na Cook, akielezea kwamba licha ya kuzidiwa na saratani, bado ana uwezo wa kufanya mashauri zaidi kwa niaba ya mwanawe.

Kisha Dk Onuoha alipokea barua pepe, ambayo aliyetazamiwa kuipokea akiwa na jina la "Brian", na ambayo ilifanya kejeli kuhusu lugha aliyoitumia katika kuelezea hali yake ya afya.