Serena Williams asubiri kujua iwapo ataadhibiwa kwa kumfokea mwamuzi Eva Asderaki

Serena Williams, Jumatatu, atafahamishwa kama ataadhibiwa kwa kumkasirikia na kumfokea mwamuzi Eva Asderaki katika fainali ya mchezo wa tennis, US Open, mjini New York.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Huenda akaadhibiwa kwa kumfokea mwamuzi Eva Asderaki

Mpinzani wake, Sam Stosur, alishinda kwa 6-2 6-3, baada ya Williams kuchukuliwa hatua na mwamuzi huyo kutoka Ugiriki.

Afisa wa pili aliyehusika, refa Brian Earley, sasa lazima aamue ikiwa atamchukulia hatua Serena, mshindi wa mapambano 13 ya Grand Slam.

Williams, mwenye umri wa miaka 29, tayari anaendelea na adhabu aliyopewa ya miaka miwili, kutokana na kupaaza sauti na kulalamika katika mashindano mengine makubwa ya Grand Slam, mwaka 2009.

"Uamuzi wowote utakaochukuliwa dhidi ya Serena Williams kukiuka sheria za Grand Slam bila shaka zitazingatia uzito wa tukio lenyewe", ilieleza taarifa ya chama cha mchezo wa tennis nchini Marekani.

"Uamuzi huo utatangazwa na mkurugenzi wa mashindano makubwa ya Grand Slam."