Patrick Makau aandikisha rekodi mpya kwa upande wa wanaume katika mashindano ya marathoni ya Berlin kwa kukimbia muda wa saa mbili, dakika tatu na sekunde thelathini na nane

Patrick Makau alifanikiwa kuhifadhi ubingwa wake katika mbio za Berlin kwa upande wa wanaume, huku akiandikisha rekodi mpya ya dunia pia katika mbio hizo

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Anyoa sekunde 21 ya Gebresellasie na kuandikisha rekodi mpya Berlin

Mkenya huyo alimaliza mbio katika muda wa saa mbili, dakika tatu na sekunde 38, akipunguza sekunde 21 kutoka rekodi ya awali iliyoshikiliwa na mwanariadha wa Ethiopia, Haile Gebrselassie, na iliyoandikishwa katika mashindano hayohayo ya Berlin, Ujerumani.

Gebresellasie wakati huu alishindwa kumaliza mbio hizo, kutokana na matatizo ya tumbo, baada ya kilimita 27.

"Asubuhi mwili wangu hakuwa katika hali nzuri sana, lakini mara tu baada ya kuanza mbio, nilianza kuhisi mwili ulikuwa katika hali nzuri. Kisha nilianza kufikiria juu ya kuvunja rekodi," alieleza Makau.

"Sikupata matatizo katika mbio hizo. Mwaka jana, viatu vyangu vilinipa matatizo, lakini leo kila kitu kilikwenda sawa kabisa".

Gebrselassie, mwenye umri wa miaka 38, na bingwa wa Olimpiki katika mbio mbili za mita 10,000, alikuwa na nia pia ya kuimarisha muda wake na kujiweka katika hali nzuri zaidi ya kufuzu kwa mashindano ya Olimpiki, akitazamia ushindani mkali kutoka kwa wanariadha wa Ethiopia kuhitimu.

Alipotambua mpinzani wake Gebresellasie alikuwa amelemewa, Makau aliongeza kasi na kuandikisha rekodi mpya.