Carlos Tevez kujitetea

Carlos Tevez Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Tevez kupata fursa ya kujitetea

Mshambulizi wa klabu ya soka ya Manchester City ya England, Carlos Tevez anatazamiwa kujitetea kuhusiana na madai kwamba alisusia mechi ya klabu bingwa kati ya timu yake na Bayern Munich ya Ujerumani.

City ilianzisha uchunguzi kufuatia madai hayo, na kumsitisha mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 27, kufuatia malalamiko kwamba alikataa kucheza alipoulizwa kufanya hivyo, katika uwanja wa Allianz Arena, mwezi Septemba.

Kupitia taarifa, Manchester City ilieleza: "Carlos Tevez anawajibika kujitetea, kufuatia kukiuka mkataba.

"Itabidi kujitetea kulingana na hatua za nidhamu zinazotazamiwa. Kesi hiyo itasikilizwa hivi karibuni".

Klabu kimeamua pia kwamba Carlos atahitajika uwanjani kwa mazoezi kuanzia Alhamisi.

Katika uwanja wa mazoezi wa City wa Carrington, afya ya mchezaji huyo itakaguliwa, na kisha kufanya mazoezi kando, pasipo kujumuika na wachezaji wenzake katika timu ya kawaida ya wachezaji 11.

Katika pambano hilo la Bayern Munich ambalo Manchester City ilishindwa magoli 2-0, Roberto Mancini mara baada ya mechi alifoka na kusema: "Alikataa kuingia uwanjani. Ikiwa ni mimi nitakayeamua, nitamtupa nje. Nimemalizana naye".

Lakini katika taarifa iliyotolewa siku ya pili, Tevez alisema hali hiyo ilitokana na hali ya "kutoelewana" na "vurugu" kutoka benchi ya wachezaji wa zamu.

Inaaminika Tevez bado ameshikilia msimamo huo.

City ilimsitisha Tevez kucheza kwa kipindi cha wiki mbili, licha ya kuendelea kupokea malipo kamili, na huku uchunguzi ukiendelea.