Ratiba ya awali ya 2013 yatolewa

Shirikisho la Soka barani Afrika Caf limetangaza mechi za awali za kuwania kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika 2013.

Baada ya vigogo kadhaa kushindwa kufuzu kucheza fainali za 2012, kuna mechi muhimu mapema katika ratiba hiyo.

Mabingwa mara saba, Misri watapambana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku Cameroon ikipambana na Guinea-Bissau.

Nigeria itapambana na Rwanda. Timu hizo mbili zinasaka kocha mpya.

Mechi za 2013 zinatokana na kubadilsiha ratiba ya michuano hiyo kutoka miaka witiri kwenda miaka shufwa na hivyo kufanya kuwepo kwa mwaka mmoja tu wa kufanya maandalizi.

Hii inamaanisha kutakuwa na muda mfupi kwa nchi zitakazofuzu kucheza fainali za 2012 kujiandaa kwa ajili ya michuano ijayo.

Ngwe ya mechi za awali itaanza na nchi ambazo zitashindwa kufuzu kucheza michuano ya Gabon na Equatorial Guinea mwezi Januari 2012.

Nchi kumi na tano ambazo zitafuzu katika ngazi ya awali zitapangwa kucheza dhidi ya timu kumi na tano zitakazocheza michuano ya 2012.

Afrika Kusini inaingia moja kwa moja kwa kuwa ni nchi itakayoandaa michuano hiyo, baada ya kuchukua nafasi ya Libya, ambayo sasa itaandaa michuano ya 2017.

Timu zote 16 zitakazopambana nchini Equatorial Guinea na Gabon mwaka 2012 zitaondolewa kwenye raundi ya mwisho ya zitakazofuzu.

Kwa kuanza Ushelisheli itacheza na Swaziland na Sao Tome kupambana na Lesotho kuwania kuingia katika droo ya awali.

Halafu kuna michuano 14 ya kuamua nani anasonga mbele kwenda raundi ya mwisho, ambapo timu hizo 16 zilizofuzu kucheza 2012 zitajiunga kuwania kucheza michuano ya 2013.

Mechi za ufunguzi za michuano ya kufuzu kucheza 2013 zitaanza mapema 2012 na raundi ya mwisho ya kufuzu itachezwa miezi ya Septemba na Oktoba mwakani.

Raundi ya kwanza ya awali:

Seychelles v Swaziland

Sao Tome v Lesotho

Raundi ya pili ya awali:

(Timu za Afrika Mashariki zenye maandishi yaliyokoza wino)

Ethiopia v Benin

Rwanda v Nigeria

Congo Brazzaville v Uganda

Burundi v Zimbabwe

Algeria v The Gambia

Kenya v Togo

Sao Tome/Lesotho v Sierra Leone

Guinea Bissau v Cameroon

Chad v Malawi

Seychelles/Swaziland v DR Congo

Tanzania v Mozambique

Central African Republic v Egypt

Madagascar v Cape Verde

Liberia v Namibia