Ferguson akubali kadi aliyooneshwa Vidic

Sir Alex Ferguson Haki miliki ya picha PA
Image caption Sir Alex Ferguson

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema anaelewa kwa nini mlinzi wa timu yake Nemanja Vidic alioneshwa kadi nyekundu na kutolewa nje wakati walipoishinda Otelul Galati.

Vidic alioneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi wa Ujermani Felix Brych baada ya kumfanyia rafu Gabriel Giurgiu katika kipindi cha pili wakati Manchester United iliposhinda nchini Romania kwa mabao 2-0.

Ferguson amesema: "Ninaweza kuelewa namna mwamuzi alivyotafsiri rafu ile.

"Huenda ni rafu tofauti na zinazochezwa Ujerumani, lakini nadhani ilikuwa adhabu kali kiasi. Ilikuwa amuoneshe kadi ya manjano."

Vidic, ambaye alikuwa amerejea katika kikosi cha Manchester United baada ya kuwa nje kwa muda akiuguza goti, sasa hataweza kucheza mechi moja ya Ubingwa wa Ulaya.

Hata hivyo kutokana na hali iliyomkumba Wayne Rooney kusimamishwa kucheza fainali za Ubingwa wa nchi za Ulaya majira yajayo ya kiangazi, Uefa huenda ikamuongezea adhabu Vidic ya kutocheza mechi mbili au tatu, hii ina maana atakosa mechi zilizosalia za Ubingwa wa vilabu vya Ulaya katika kundi lao la C.

Ferguson ameongeza: "Niliangalia kwa makini, mguu wake ulikuwa juu kiasi."

Ushindi huo mjini Bucharest, uliotokana na mabao mawili ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Rooney kwa mikwaju ya penalti, umeipatia United mafanikio ya kwanza katika kuwania Ubingwa wa Ulaya msimu huu kufuatia sare mara mbili katika mechi zake za awali za ufunguzi dhidi ya Benfica na FC Basel.