Gerrard alikuwa na hofu kama angecheza

Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard amekiri alikuwa na wasiwasi iwapo angerejea uwanjani na kuweza kucheza soka tena, baada ya kuumia wakati wa "kipindi kigumu cha miezi sita".

Haki miliki ya picha AP
Image caption Steven Gerrard

Gerrard, mwenye umri wa 31, alifunga bao walipocheza na Manchester United siku ya Jumamosi katika mechi yake ya kwanza kuanza kucheza tangu mwanzo kufuatia upasuaji aliofanyiwa chini ya nyonga mwezi wa Machi.

Alipoulizwa iwapo alikuwa na wasiwasi wa kupotea kipaji chake, Gerrard alisema: "Nadhani ni jambo la kawaida kuwa na wasiwasi na mawazo tofauti huwa yanakujia kichwani.

"Kulikuwa na wakati nilikuwa chini kuliko ilivyowahi kunitokea katika kipindi changu cha usakataji kandanda."

Gerrard amesema kabla ya upasuaji ilikuwa lazima achomwe sindano ili aweze kucheza mechi.

"Kimsingi nilikuwa nafahamu hiyo haikuwa sawa," aliongeza.

"Unaweza kufanya hivyo kwa nyakati fulani tu kabla mwili wako kuanza kushindwa kuhimili na mwili wangu ulishindwa kuhimili."

"Nilikuwa nafahamu hali ingekuwa mbaya, jambo ambalo sikuwa nimelizoea. Nilijaribu kadri ya uwezo wangu kutoonesha hisia lakini nakiri sikuwa katika hali yangu ya kawaida."

Gerrard alitarajiwa kurejea uwanjani mwanzoni mwa msimu lakini akakumbwa na maambukizi yanayohusiana na majeraha chini ya nyonga mwezi wa Julai. Alilazwa hospitalini kwa matibabu.