Liverpool kunufaika na klabu ya Uruguay

Liverpool inakaribia kukamilisha mkataba na mabingwa wa kandanda wa Uruguaya Nacional utakaowapatia nafasi ya kwanza kuchagua wachezaji nyota chipukizi wa klabu hiyo ya Uruguay.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Luis Suarez

Klabu ya Liverpool inataka kutega nyavu katika chuo ambacho kimetoa wachezaji nyota wawili wanaochezea klabu hiyo kwa sasa, Luis Suarez na Sebastian Coates.

Msemaji wa klabu ya Nacional amekiambia kitengo cha michezo cha BBC: "Liverpool watakuja na kuangalia namna chuo chetu kinavyoendeshwa na watakuwa na nafasi ya kwanza kuwasajili wachezaji wetu chipukizi watakaowahitaji.

"Kwa sasa tunakamilisha makubaliano hayo haraka iwezekanavyo."

Klabu ya Nacional yenye makazi yake mjini Montevideo, imepiga hatua kubwa kufufua soka ya Uruguay.

Wachezaji 14 walioshiriki na kunyakua kombe la mwaka huu la Copa Amerika katika kikosi cha nchi hiyo kilichokuwa na wachezaji 23 ama wanachezea Nacional au walikuzwa na klabu hiyo.

Klabu hiyo imeweka watu wanaopiga doria nchi nzima ama maskauti, kutafuta vijana wenye vipaji vya kusakata kandanda kwa ajili ya kuwaingiza katika chuo chao, ambacho kwa sasa kinafundisha wachezaji 120 wenye umri wa kati ya miaka 13 na 20.

Suarez, mwenye umri wa miaka 24, ametokea katika chuo cha soka cha Nacional kabla hajajiunga na klabu ya Uholanzi ya Groningen na baadae akaelekea Ajax.

Alisajiliwa na klabu ya Liverpool kwa kitita cha paundi milioni 22.7 mwezi wa Januari na hadi sasa ameshafunga mabao matano msimu huu.

Pia klabu hiyo mwezi wa Agosti ilimsajili mlinzi wa kati mrefu mwenye futi sita na inchi 6 Coates, baada ya kung'ara katika michezo ya Copa America.

Wachezaji hao wawili wa Uruguay ni sehemu ya wachezaji kutoka Amerika Kusini wanaochezea Liverpool akiwemo Mbrazil Lucas Leiva na Maxi Rodriguez kutoka Argentina.

Baada ya kumchukua Coates, mkurugenzi wa soka wa Liverpool Damien Comolli amesema wana nia kubwa kuimarisha uhusiano na klabu ya Nacional.

Msemaji wa Liverpool amesema klabu yao kwa sasa haina la ziada la kuongeza kutokana na maoni ya Comolli.