Carling Cup: Man City yafanya mauaji tena

Mancini Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kipigo kingine... Mancini

Manchester City imeingia katika nane bora ya Kombe la Carling kwa kuizaba Wolves mabao 5-2.

Wolves wakicheza nyumbani ndio walianza kupata bao kupitia Nenad Milijas. Hata hivyo Adam Johnson alisawazisha goli hilo.

Dakika nne baadaye Samir Nasri aliandika bao la pili baada ya kuunganisha mpira uliopigwa na Johnson, kabla ya Edin Dzeko kuandika bao la tatu.

Dorous De Vries wa Wolves alijifunga mwenyewe na Dzeko tena kufunga bao la tano.

Jamie O'Hara alipachika bao la pili la Wolves baada ya kuunganisha krosi ya Stephen ward.

Kwingineko Liverpool iliponea chupuchupu baada ya kuifunga Stoke City 2-1.

Luis Suarez alifanya juhudi binafsi na kupata magoli yote mawili, baada ya Liverpool kufungwa bao kupitia Kenwyne Jones muda mfupi kabla ya mapumziko.

Suarez alipachika mabao hayo katika dakika za 54 na 85.