Adebayor hajuti kuondoka Manchester City

Emmanuel Adebayor amesisitiza hajuti kuondoka klabu ya Manchester City na kuelezea muda aliokuwa katika klabu hiyo "alisumbuka".

Haki miliki ya picha PA
Image caption Emmanuel Adebayor

Adebayor alijiunga na Tottenham kwa mkopo wa muda mrefu mwezi wa Agosti baada ya kuonekana haendani na mipango ya Roberto Mancini tangu mwezi wa Desemba mwaka jana.

Amekiambia kipindi cha michezo cha BBC: "Nawatakia kila la heri, lakini sifikirii kuwa sehemu ya kikosi hicho kwa sasa.

"Kila nilipokuwa naamka asubuhi mwaka jana kwa ajili ya kwenda mazoezini ilikuwa ni mashaka matupu."

Kikosi chenye wachezaji ghali cha Mancini kwa sasa ndio kinashikilia usukani wa Ligi Kuu ya England bila ya Adebayor, lakini mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal amesema kamwe hajihisi mpweke bila kutokuwepo Manchester City baada ya kuzoea haraka mazingira mapya kaskazini mwa London.

"Hata kama nyumba ni hekalu, unatakiwa kupendwa na unatakiwa kuwa mwenye furaha."

Adebayor alikataa kuzungumza chochote moja kwa moja kuhusu Mancini, lakini inaonekana dhahiri uhusiano baina ya watu hao umevunjika. Hii imetokana na namna anavyomsifia meneja wake mpya.

"Harry Redknapp ni meneja mzuri sana," Adebayor aliongeza.

"Anajua kuzungumza na wachezaji. Unahitaji imani kama hiyo kutoka kwa meneja wako. Anakukubalia utoke na ufanye mambo yako. Hii ndio maana Harry ana vitu wengine wanavikosa.

Adebayor ameshafunga mabao matatu katika mechi sita alizocheza msimu huu na kuisaidia Tottenham kusogelea eneo la timu nne bora za ligi wakiwania kwa mara nyingine kucheza Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.