Tottenham yapanda hadi nafasi ya tano

Gareth Bale alifanikiwa kufunga mabao mawili walipoilaza Queens Park Rangers mabao 3-1 na kuifanya Tottenham kutopoteza mchezo katika michezo saba waliyocheza.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Gareth Bale

Katika mchezo uliomilikiwa kwa kiasi kikubwa na Spurs, Bale aliachia mkwaju wa yadi 18 baada ya kumegewa pasi murua na Aaron Lennon.

Rafael van der Vaart baadae akaweza kuvunja mtego wa kuotea na kuachia mkwaju uliompita mlinda mlango wa QPR Paddy Kenny baada ya kuuwahi mpira uliokuwa umepigwa na Ledley King.

QPR walichachamaa kipindi cha pili na Jay Bothroyd aliyeingia kipindi hicho aliweza kurudisha uhai kwa timu yake kwa kufunga bao la kichwa karibu kabisa na lango.

Bao la tatu la Tottenham lililowahikishia ushindi lilipachikwa tena na Gareth Bale katika dakika ya 72.

Matokeo hayo yameifikisha Tottenham hadi nafasi ya tano ya msimamo wa ligi wakiwa wamefungana pointi na Chelsea na Newcastle.