Mancini tayari kumrejesha Tevez

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amesema Carlos Tevez anaweza kurejea katika kikosi chake iwapo ataomba radhi kutokana na vitendo vyake ambavyo vilivyosababisha klabu imsimamishe.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Roberto Mancini na Carlos Tevez enzi walizokuwa wakipatana

Tevez hajachaguliwa katika kikosi cha Man City tangu Mancini amtuhumu kwa kugoma kucheza dhidi ya Bayern Munich mwezi wa Septemba, tuhuma ambazo Tevez amezikanusha.

Lakini katika mahojiano na gazeti la Italia la Corriere della Sera, Mancini amesema: "Kila kitu kinategemea na Carlos mwenyewe."

"Iwapo ataomba radhi kwa kikosi na kwangu basi kila kitu kitakuwa kama ilivyokuwa zamani."

Mancini, ambaye timu yake inapambana na Villarreal nchini Hispania siku ya Jumatano usiku, aliongeza: "Iwapo hataomba radhi, basi Tevez ana thamani ambayo kila mtu anaifahamu na kuna jambo litatokea mwezi wa Januari."

Baada ya mechi na Bayern, Mancini alisema Tevez "amekwisha" katika City, huku mshambuliaji huyo wa Argentina akiwa hajasimamishwa wakati klabu ikiwa inafanya uchunguzi wa ndani.

Mwezi wa Oktoba, klabu ilimkuta na hatia ya kuvunja kanuni tano za mkataba wake, ikiwemo kucheza katika mechi yoyote ambapo mchezaji atachaguliwa na klabu huku akielekezwa na afisa wa klabu".

City ilimtoza faini ya mshahara wa wiki nne, lakini ililazimishwa kupunguza ukali wa adhabu hiyo na kuwa mshahara wa wiki mbili baada ya Chama cha Wanakandanda wa Kulipwa (PFA).

Tevez anatazamiwa kukata rufaa dhidi ya kufungiwa kucheza na anafikiria kumshitaki Mancini kwa kumchafulia jina.

"Alikuwa hakujiandaa kabisa na alishauriwa vibaya," alisema Mancini. "Sipendelei hali iendelee kuwa hivi na nitakuwa wa kwanza kumsamehe."