Ufisadi haujaenea katika kriketi

Afisa mkuu wa kupambana na ufisadi katika bodi ya kriketi, Sir Ronnie Flannagan, amesema uovu huo haujaenea katika mchezo wa kiriketi, kama inavyofikiriwa na wengi.

Matamshi ya afisa huyo ni kufuatia wachezaji watatu wa Pakistan kupewa hukumu ya kufungwa jela kwa kupanga matokeo ya mechi.

Sir Ronnie Flannagan amesema: "Ufisadi bila shaka haujaenea katika ulimwengu wa kriketi.

"Nadhani wanaohusika ni watu wachache sana."

Flannagan, ambaye ni afisa mkuu wa kupambana na ufisadi na anayehusiana pia na masuala ya usalama katika baraza la mchezo huo la ICC, aliongezea: "Wengi ya wapenzi wa kriketi ni watu wanaozingatia maadili".

Image caption Wachezaji na wakala waliokabidhiwa hukumu ya kufungwa jela

Akitoa hukumu kwa wachezaji na wakala wao, awali Jaji Cooke amesema haikuwa mchezo wa kriketi tu uliowekwa kwenye kitendawili, ni athari za ndani zaidi za vitendo vyao katika taaluma ya mchezo huo ambazo zinafanya makosa yao kuwa makubwa.

Amewaambia Mazhar Majeed na Salman Butt kuwa wamehusika zaidi na kula njama ya kupanga matokeo ya mchezo huo.

Majeed amehukumiwa kwenda jela miaka 2 na miezi 8, na nahodha wa zamani Butt miaka miwili na nusu.

Jaji huyo amesema hukumu yake inaonyesha ukweli kuwa Butt alimpa rushwa Amir, kijana mdogo ambaye amehukumiwa jela miezi sita kwa kosa hilo.

Mwenzake Mohammad Asif amehukumiwa mwaka mmoja kwa kula njama za kupanga matokeo wakati wa michuano ya michezo ya Lords mwaka jana.

Mawakili wa Amir na Butt wameonyesha dalili ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.