Barua ya vitisho atumiwa Anton Ferdinand

Anton Ferdinand na John Terry wakizozana Haki miliki ya picha PA
Image caption Anton Ferdinand na John Terry wakizozana

Polisi wa Uingereza wanachunguza barua ya vitisho iliyotumwa kwa mchezaji wa QPR Anton Ferdinand.

Maafisa wa Polisi wa Metropolitan wamekataa kueleza kilichoandikwa katika barua hiyo aliyotumiwa Ferdinand au lini walipokea malalamiko kuhusiana na barua hiyo.

Msemaji wa Polisi amesema: "Naweza kuthibitisha maafisa wetu wanachunguza juu ya tuhuma hizo za vitisho zilizotumwa kwa njia ya barua."

Ferdinand yupo katika mzozo unaohusiana na tuhuma za kutupiwa maneno ya kibaguzi na nahodha wa Chelsea na England John Terry, wakati QPR ilipocheza na Chelsea, tuhuma ambazo Terry amezikanusha.

Polis na Chama cha Soka cha England - FA, wanachunguza madai hayo ya kauli za kibaguzi, ambazo Ferdinand anadai Terry alimtamkia mwezi wa Oktoba katika uwanja wa Queens Park Rangers wa Loftus Road.