Joe Frazier afariki dunia

Bingwa wa zamani wa ngumi uzito wa juu duniani Joe Frazier amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi saratani ya ini, familia yake imesema.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Joe Frazier alipotwangana na Mohammad Ali mwaka 1971

Frazier - pia alijulikana kwa jina la Smokin' Joe - alikuwa akitibiwa katika nyumba ya wagonjwa mahututi huko Philadelphia baada ya kugunduliwa anaugua saratani wiki kadha zilizopita.

Bingwa huyo wa zamani aliyekuwa na umri wa miaka 67 alikuwa mtu wa kwanza kumchapa Muhammad Ali mwaka 1971, lakini katika mapambano mawili yaliyofuatia alitwangwa na Ali.

Alishikilia taji la ubingwa ndondi za uzito wa juu duniani kati ya mwaka 1970 na 1973.

Frazier alishinda medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki mwaka 1964 wakati aliposhiriki michezo hiyo alipochukua nafasi ya mwanamasumbwi Buster Mathis, aliyemchapa katika mchezo wa majaribio lakini hakuweza kushiriki michezo hiyo kutokana na kuumia.

Alishinda taji la ubingwa wa dunia mwaka 1970, baada ya Ali kupokonywa ubingwa wake mwaka 1967 kwa kukataa kupigana vita vya Vietnam, kwa kumtwanga Jimmy Ellis mjini New York.

Miaka mitatu baadae alipoteza taji la ubingwa wa dunia alipopigwa na George Foreman.

Lakini mwanamasumbwi huyo sifa zake zinajulikana zaidi kwa mapambano matatu ya kukata na shoka dhidi ya Ali, likiwemo la mwaka 1975 lililopewa jina la "Thrilla in Manila".

Mabondia hao wawili walikuwa na uhusiano mbaya kutokana na kauli za kejeli alizokuwa akitumia Ali kabla ya mapambano yao.

Lakini katika miaka ya karibuni, iliarifiwa walikuwa na uhusiano mzuri.

"Dunia imempoteza bingwa mashuhuri. Kila mara nitamkumbuka Joe kwa heshima zote kutokana na kuvutiwa naye, alisema Ali, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 69.

"Salamu zangu za rambirambi nazituma kwa familia yake na wale waliompenda."

Frazier alistaafu masumbwi mwaka 1976 baada ya kuchapwa kwa mara nyingine na Foreman. Baadae mwaka 1981 alijaribu kurejea ulingoni bila mafanikio, akipigana mara moja tu kabla ya kutundika glovu zake.

"Usiku mwema Joe Frazier. Nakupenda rafiki mpenzi," alisema Foreman kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

Bingwa wa zamani wa uzito wa juu duniani Muingereza Lennox Lewis ameiambia BBC: "Bila yeye, mabingwa wengine wa ngumi wasingekuwa mashuhuri kwa sababu walikuwa wakiiga mbinu zake za kupigana.