Blatter adai "hakuna" ubaguzi uwanjani

Mlinzi wa England na Manchester United Rio Ferdinand amesema ameshangazwa na madai ya Sepp Blatter kwamba hakuna tatizo la ubaguzi katika mchezo wa kandanda uwanjani.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais wa Fifa Sepp Blatter ajichanganya kuhusu ubaguzi

Rais wa Fifa amesema matukio ya uwanjani yanaweza kutatuliwa kwa kupeana mikono, ingawa baadae alidai ameeleweka vibaya.

"Nieleze nimesoma matamshi ya Blatter vibaya... iwapo sijakosea basi nimeshangazwa," alisema Ferdinand kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

Ferdinand baadae alimtumia ujumbe kwa Blatter. Katika ujumbe huo aliandika: "Matamshi yako kuhusiana na ubaguzi yanashangaza na kwa kweli yanachekesha. Iwapo mashabiki watapaza sauti zao kwa maneno ya kibaguzi jee kushikana mikono hapo ni sawa?"

Matamshi ya Blatter yamekuja wakati nahodha wa Chelsea John Terry akichunguzwa na polisi pamoja na Chama cha Soka cha England juu ya tuhuma za kumtamkia maneno ya kibaguzi mlinzi wa QPR Anton Ferdinand, ambaye ni mdogo wake Rio.

Mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez naye ameshtakiwa na FA kwa tuhuma za kutoa maneno ya kibaguzi dhidi ya mchezaji mwenzake Ferdinand katika Manchester United, Patrice Evra.

Alipoulizwa iwapo anadhani ubaguzi uwanjani ni tatizo katika soka ya kisasa, Blatter aliiambia televisheni ya CNN kipindi cha michezo: "Nakanusha hilo. Hakuna ubaguzi.

"Huenda kuna tatizo la mchezaji mmoja kwa wengine - anakuwa anasema kitu ambacho kinakuwa si sahihi.

"Lakini yule ambaye anaathirika na hilo, hana budi kusema ndio mchezo. Tumo katika mchezo na mwishoni mwa mchezo, tunapeana mikono na hili linawezekana, kwa sababu tumefanya kazi kubwa kupambana na ubaguzi."