Suarez ashtakiwa kwa kashfa ya ubaguzi

Mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez ameshtakiwa na Chama cha Kandanda cha England -FA- kwa kumtolea maneno ya kibaguzi mlinzi wa Manchester United Patrice Evra.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Luis Suarez na Patrice Evra walipozozana

Wachezaji hao wawili walikwaruzana tarehe 15 mwezi wa Oktoba timu hizo zilipotoka sare ya 1-1 mchezo uliochezwa uwanja wa Liverpool wa Anfield.

Suarez anayechezea pia timu ya taifa ya Uruguay, amekanusha kutumia maneno ya kibaguzi dhidi ya Evra.

Kufuatia mashtaka hayo ya FA, klabu ya Liverpool imesema itaendelea kumuunga mkono Suarez na ataendelea kukanusha mashtaka hayo atakaporejea kutoka mechi za kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na FA imesema: "Inatuhumiwa kwamba Suarez alitumia lugha ya kibaguzi, matusi ama maneno ya kejeli dhidi ya mchezaji wa Manchester United Patrice Evra kinyume na kanuni za FA.

"Inadaiwa zaidi hii ni pamoja na kutaja asili ya mtu, rangi au utaifa wa Patrice Evra."

Hivi karibuni meneja wa Liverpool Kenny Dalglish alisema haamini kwamba ubaguzi upo ndani ya klabu yake.

Taarifa iliyotolewa na klabu ya Liverpool baada ya FA kutangaza inamshitaki Suarez imesema: "Klabu jioni hii imepokea barua kutoka Chama cha Kandanda kwa uamuzi wake wa kumshtaki Luis Suarez na itachukua muda kupitia kwa makini nyaraka zilizotumwa kwetu.

"Tutazungumza naye kwa kina atakaporejea kutoka katika mechi za kimataifa, lakini atakanusha mashtaka yanayomkabili na tunatazamia ataomba shauri hilo lisikilizwe.

"Luis bado ana nia ya kusafisha jina lake kutokana na tuhuma zinazomkabili za kutolea maneno ya kibaguzi Patrice Evra.

Evra alilalamika mara tu baada ya mechi na alinukuliwa na Televisheni ya Ufaransa ya Canal Plus akisema: "Kuna kamera, utaweza kuona Suarez akinitamkia maneno fulani takriban mara kumi."

Suarez mapema mwezi huu alisema kupitia vyombo vya habari vya Uruguay: "Hakuna ushahidi kama nilisema neno lolote la kibaguzi kwa Evra. Hakuna kitu kama hicho.

"Kulikuwa na mazungumzo ya aina mbili, kwa Kihispania na pili kwa Kiingereza. Sikumtukana. Ilikuwa ni njia yangu ya kujieleza. Nilimwita kitu ambacho wachezaji wenzake wa Manchester wanamuita na hata wao walishangaa kutokana na alivyokasirika."

Evra alitoa taarifa mara tu baada ya mchezo kwa mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo Andre Marriner ambaye alijumuisha madai hayo kwenye ripoti yake.