Redknapp aamini Spurs itashinda ubingwa

Harry Redknapp anaamini Tottenham inaweza kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu iwapo wataendelea kucheza katika kiwango cha sasa.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Harry Redknapp anaamini Tottenham itanyakua ubingwa

Spurs imesogea hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi baada ya kuilaza Aston Villa 2-0 katika uwanja wa White Hart Lane na sasa katika michezo tisa ya ligi waliyocheza wameshinda minane.

Meneja Redknapp alisema: "Uwezekano wa kunyakua ubingwa upo, ni jambo linalowezekana. Iwapo utaendelea kushinda michezo na kujiamini utafanikiwa.

"Iwapo tutacheza kwa kiwango hiki, tutashinda ligi, lakini itakuwa kazi ngumu."

Redknapp alisema ushindi dhidi ya Villa, uliopatikana kutokana na mabao aliyofunga Emmanuel Adebayor, anayechezea timu hiyo kwa mkopo, yalikuwa "dawa bora" kwake ya kurejea kuifunza timu hiyo baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Wakati huo huo, Villa kwa sasa wameshinda mchezo mmoja tu katika mechi tano za Ligi Kuu ya England walizocheza.