Villa-Boas atozwa faini paundi 12,000

Chama cha Soka cha England kimemtoza faini meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas ya paundi 12,000, baada ya kutoa matamshi ya makali wakati timu yake ilipofungwa bao 1-0 na QPR.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Andre Villas-Boas atozwa faini paundi 12,000

Meneja huyo wa Chelsea alimtolea maneno makali mwamuzi Chris Foy, ambaye aliwatoa nje kwa kuwaonesha kadi nyekundu Jose Bosingwa na Didier Drogba na pia aliipatia QPR adhabu ya mkwaju wa penalti.

Wachezaji saba wa Chelsea katika mchezo huo pia walioneshwa kadi ya manjano na klabu hiyo imetozwa faini ya paundi 20,000.

Villas-Boas awali alikanusha mashtaka yaliyokuwa yakimkabili lakini alipatikana na hatia na kuonywa kuchunga vitendo na kauli zake siku zijazo.

Akizungumza baada ya mchezo uliofanyika mwezi wa Oktoba katika uwanja wa Loftus Road wa QPR, Villas-Boas alisema: "Mwamuzi alikuwa ovyo, ovyo ovyo sana na ndio amesababisha matokeo haya.

"Nilizungumza naye baada ya mchezo na nilimtolea maneno makali. Sijali kama yupo sawa au la.

Villas-Boas, mwenye umri wa miaka 34, alichagua kutokiri makosa yake mbele ya tume ya maadili ya Chama cha Soka.