Ivory Coast vinara wa soka Barani Afrika

Ivory Coast imekwea kileleni mwa timu bora za kandanda Barani Afrika kutokana na viwango vipya vya ubora vinavyotolewa na Fifa kila mwezi kuonesha jinsi nchi zilivyofanya vizuri au kuporomoka.

Image caption Ivory Coast yapanda kileleni kwa ubora wa kandanda Afrika

Tembo hao wa Afrika Magharibi katika ubora wa viwango vya soka duniani wanashikilia nafasi ya 16, wakati Ghana ipo nafasi ya pili kwa ubora Afrika na kwa dunia nafasi ya 29.

Wafalme wa kandanda Duniani na Ulaya, Hispania wameendelea kushikilia nafasi ya kwanza duniani, licha ya hivi karibuni kufungwa na England katika mchezo wa kirafiki.

Ivory Coast inaziongoza Black Stars ya Ghana na Mabweha wa Jangwani timu ya taifa ya Algeria.

Misri, Nigeria, Senegal, Cameroon, Afrika Kusini, Cape Verde na Tunisia wanakamilisha nafasi 10 bora barani Afrika.

Wakati huo huo, England imesogea hadi nafasi tano kwa ubora duniani kufuatia ushindi wake wa mechi za kirafiki hivi karibuni dhidi ya Hispania na Sweden.

Uholanzi inashikilia nafasi ya pili lakini Ujerumani katika nafasi ya tatu imeziba pengo kwa karibu baada ya kuishinda Uholanzi mabao 3-0.

Mabingwa wa soka wa Amerika Kusini, Uruguay imezikaribia timu zinazoshika nafasi tatu za juu, kwa kushika nafasi ya nne hasa baada ya kuilaza Chile hivi karibuni katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2014.

Upimaji huo wa viwango vya usakataji wa kandanda unatokana na michezo yote ya kimataifa katika mzunguko wa miaka minne.

Fifa inachukulia michezo 131 iliyochezwa katika mwezi uliopita, ikiwemo ile 72 ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.