Mwanariadha mlemavu apona

Mwanariadha mlemavu ambaye amewahi kushinda mashindano kadhaa ya kuendesha baiskeli za walemavu ameweza kutumia tena miguu yake iliyopooza kwa miaka 13.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Monique van der Vorst

Tukio hili lilitokea baada ya Monique van der Vorst kugongana na baiskeli nyingine wakati wa mashindano na ajali hiyo kuzua hofu kwamba huenda ikamzidishia hatari ya viungo vyake, badala yake alianza kuhisi uhai katika miguu yake.

Kabla ya ajali hiyo Monique aliwakilisha Uholanzi mjini Beijing mwaka 2008 na kushinda medali mbili katika mashindano ya kutumia mikono.

Hivi sasa Bi Monique amepata nafasi katika timu ya Uholanzi ya wanariadha wasio walemavu akidhamiria kushiriki mbio za barabara za mwaka 2016 katika Olimpiki za mjini Rio, Brazil.

Bibi huyo kutoka Uholanzi akiwa na umri wa miaka 27 amesema nia yake ni kushiriki mashindano ya wasio walemavu.

Akiwa mwenye umri wa miaka 13, Van der Vorst alipooza miguu yote miwili baada ya kufanyiwa upasuaji wa magoti, jambo lililokua la kawaida.

Tangu hapo ikabidi atumie gari la walemavu, na wakati akipewa ushauri nasaha ndipo alipodokezewa kuhusu gari la kutumia mikono na hivyo hatomtegemea mtu mwingine kumtembeza.

Huo ukawa mwanzo wake kutumia baiskeli na kufanikisha mapenzi yake ya kushindana na punde akajikuta amekua bingwa wa Dunia na wa Ulaya mara kadhaa.

Mnamo mwaka 2008, alipatwa na ajali ya barabarani iliyomuathiri uti wa mgongo na kupooza kuanzia kiunoni hadi miguuni.

Hata hivyo alishiriki mashindano ya Olimpiki za walemavu mjini Beijing mnamo mwaka 2009 ambako alitajwa kuwa mwanariadha mlemavu bora wa mwaka.

Mnamo mwaka 2010, kufuatia ajali nyingine, mara hii akigongana na mwanariadha mwenzake katika mazowezi alianza kupata hisia miguuni na kuanzia hapo akaanza kutumia miguu yake.

Wakati akijifunza kutembea, kocha mmoja alimuazima baiskeli. Kuanzia hapo amekua akifanya mazowezi na hivi sasa amejiunga na mshindi wa medali ya fedha Marianne Vos kwa mashindano ya mwezi septemba.

Meneja wa Timu ya Rabobank Jeroen Blijlevens amesema kua ana imani na mwanariadha huyo ingawa anahitaji juhudi zaidi, lakini kuwepo kwake katika kikosi cha Uholanzi kitawapa moyo wenzake.