Harambee hoi kwa Malawi

Cecafa Haki miliki ya picha
Image caption Michuano ya Cecafa inaendelea Tanzania

Timu ya taifa ya Malawi imeisambaratisha timu ya taifa ya Kenya Harembee Stars 2–0 katika mchezo wa kundi C wa michuano ya Mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki na kati CECAFA SENIOR CHALLENGE CUP uliochezwa katika uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Tanzania.

Goli la kwanza la Malawi ambayo ni mwalikwa katika mashindano hayo lilipatikana katika katika dakika ya 24 kipindi cha kwanza ambalo lililofungwa na John Banda kwa shuti kali baada ya kutokea piga ni kupige katika goli la Harambee Stars. Kipindi cha pili Timu zote zilicharuka kila moja ikajaribu kupata goli lakini Malawi ndio waliweza kuongeza goli la pili kwa njia penati ilifungwa na Joseph Kamwend baada ya golikipa wa Harambee Stars Duncan Ochieng kumshika mchezaji mmoja wa Malawi ndani ya kumi na nane. Katika mechi nyingine iliyochezwa mapema leo katika uwanja huo huo wa Taifa mjini Dar es Salaam Timu ya taifa ya Sudan imetoka sare ya 1-1 na Ethiopia katika mchezo wa kundi C. Goli la sudan lilifunguwa na Tahir Osman katika dakika ya tano ya kipindi cha kwanza. Mechi nyingine iliyochezwa Jumatatu ni ya kundi B ambayo ilifanyika katika uwanja wa Azam nje kidogo ya mji wa Dar es Salaam ambapo timu ya taifa ya Uganda The Cranes imeisambaratisha bila huruma timu ya taifa ya Somalia kwa jumla ya magoli 4 -0.

Emmanuel Okwi ambaye pia ni mshambuliaji wa Timu ya Simba ya Tanzania aliifungia timu yake ya Uganda hat trick yaani magoli matatu. Siku ya Jumanne kwenye uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam kutakuwa na mechi mbili ambapo katika mechi ya awali ya kundi A timu ya taifa ya Rwanda itamenyana na timu ya taifa ya Zimbabwe na baadae majira ya saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki Bingwa mtetezi wa kombe hilo timu ya Tanzania bara (Kilimanjaro Stars) itamenyana na timu ya taifa ya Djibout katika mchezo mwingine wa kundi A.