Je, Man City tayari ni mabingwa?

Manchester City wanaendelea kuonyesha ari ya kutaka ubingwa wa ligi kuu ya Premier msimu huu, kwa kudumisha rekodi yao nzuri ya kutoshindwa wakiwa nyumbani kwa asilimia 100, walipocheza siku ya Jumamosi na kuinyosha kikamilifu Norwich magoli 5-1.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Aguero ameandikisha bao la 13 katika ligi ya Premier msimu huu

Sergio Aguero alifunga bao lake la 13 msimu huu.

Mkwaju wa Samir Nasri kutoka yadi 35 ilikuwa vigumu kuzuilika, na akaongezea bao la pili, huku Yaya Toure akiongezea la tatu.

Steve Morison alitia wavuni bao la Norwich kwa kichwa kutoka yadi sita, lakini naye kijana mwenye vituko vingi uwanjani, Mario Balotelli, akafunga kwa kutumia bega, na Adam Johnson akaongezea bao la tano na la kumalizia kazi kwa upande wa Man City.

Man City sasa wanaongoza ligi wakiwa na pointi 38.

Katika viwanja vingine, Blackburn ilipata ushindi wa magoli 4-2 ilipocheza na Swansea.

Kitumbua cha Newcastle nacho kilipata mchanga katika mechi ya nyumbani, wakati walipofungwa magoli 3-0 walipoikaribisha Chelsea.

QPR ilipata sare ya 1-1 dhidi ya West Brom.

Timu nyingine iliyoshindwa kuwika katika uwanja wa nyumbani ni Wigan, ambayo Arsenal iliiweza nguvu kabisa kwa kuizaba magoli 4-0.

Mchezo wa mwisho Jumamosi ulikuwa ni kati ya Aston Villa na Man United, na ambao Man U ilishinda goli 1-0.