Messi, Ronaldo na Xavi nani bora

Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Xavi wametajwa katika orodha ya wachezaji watatu wa mwisho watakaowania tuzo ya Fifa iitwayo Ballon d'Or ya mchezaji bora wa soka duniani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Messi na Xavi wanawania tuzo ya Fifa ya mchezaji bora

Messi alishinda tuzo ya mchezaji bora wa kandanda duniani mwaka wa 2009 na 2010, wakati Xavi wanayecheza pamoja katika klabu ya Barcelona alishika nafasi ya pili mwaka jana.

Mpachika mabao hodari wa Real Madrid Ronaldo, mwaka 2008 ndiye alikuwa mcheza kandanda bora duniani na mara mbili ameshika nafasi ya pili.

Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney ameteuliwa kuwania tuzo ya mpachika bao la mwaka maridadi, wakati meneja wake Sir Alex Ferguson anawania tuzo ya mwalimu bora wa soka wa mwaka.

Sir Alex Ferguson yupo katika kinyanganyiro hicho pamoja na meneja wa Barcelona Pep Guardiola na wa Real Madrid Jose Mourinho.

Rooney ameteuliwa kuwania tuzo hiyo kutokana na bao lake maridadi alilofunga dhidi ya Manchester City msimu uliopita.

Pia katika orodha hiyo yupo Messi kutokana na bao lake la kuuchepua mpira alipomfunga mlinda mlango wa Arsenal Wojciech Szczesny msimu uliopita katika mchezo wa kuwania Ubingwa wa Ulaya, pamoja na bao la mshambuliaji wa Santos ya Brazil, Neymar alipofunga bao la kukata na shoka walipocheza na Flamengo mwezi wa Julai.

Messi anapewa nafasi kubwa kushinda tuzo ya Ballon d'Or kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kandanda safi aliyoionesha msimu uliopita katika klabu yake ya Barcelona, ambapo aliweza kufunga mabao 53 katika mashindano yote timu hiyo iliyocheza.

Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Argentina alikuwa mfungaji wa mabao mengi wa Barcelona na kuisaidia timu yake kutetea taji la ubingwa wa Hispania na pia kunyakua tena ubingwa wa Ulaya baada ya kuilaza Manchester United katika uwanja wa Wembley.

Xavi, ni mmoja kati ya wachezaji hodari wa kiungo duniani, amekuwa chachu ya Messi kufunga mabao mengi, wakati Ronaldo aliyefunga mabao 53 kwa klabu yake ya Real Madrid na kumaliza nafasi ya pili ya Ligi Kuu ya Hispania - La Liga na kuondolewa katika hatua ya nusu fainali ya Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Barcelona.

Kwa upande wa akina dada mshambuliaji wa Brazil Marta anatazamiwa kushinda kwa mara ya sita tuzo ya Mwanasoka Bora Mwanamke wa Mwaka, lakini anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Homare Sawa wa Japan na Mmarekani Abby Wambach.

Tuzo hiyo ya mwanasoka bora wa Fifa ya Ballon d'Or huamuliwa kutokana na kura za waandishi wa habari, makocha na manahodha wa timu za taifa.

Mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa tarehe 9 mwezi wa Januari mjini Zurich.