Liverpool yalazwa na Fulham 1-0

Bao lililofungwa na Clint Dempsey dakika za mwisho liliipatia Fulham ushindi wa 1-0 dhidi ya Liverpool waliokuwa wakicheza 10 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England na kumaliza matumaini ya Liverpool kupata ushindi wa saba mfululizo nje ya uwanja wao.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Fulham yaididimiza Liverpool 1-0

Mchezaji wa Liverpool Jay Spearing alitolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 71 wakati akiwania mpira na Moussa Dembele lakini akainua zaidi miguu yake na kuonekana amecheza rafu.

Liverpool walifungwa bao hilo katika dakika ya 85 wakati Dempsey alipopachika mpira wavuni baada ya mlinda mlango Jose Reina kuutema mkwaju wa Danny Murphy.

Mapema Jordan Henderson na Stewart Downing wa Liverpool mikwaju yao iligonga mwamba langoni kwa Fulham, wakati Dempsey wa Fulham naye alifanya hivyo hivyo.

Liverpool kucheza kwao pungufu ya mchezaji mmoja ilionekana ni faraja kwa Fulham na jitahada za Liverpool kujipapatua zilifika ukingoni baada ya Reina kufanya kosa kubwa, wakati kabla ya hapo aliokoa mikwaju mikali ya hatari iliyoelekezwa langoni kwake.

Meneja wa Fulham Martin Jol baada ya mchezo alisema: "Tulipoteza pointi nyumbani tulipocheza dhidi ya Everton wakati kikosi chetu kilipokuwa kizuri, kwa kweli hatukuwa na bahati. Usiku huu mambo yetu yamekuwa mazuri.

"Nadhani ilikuwa rafu mbaya iliyofanywa na Jay Spearing. Mguu wake ulimkwatua Dembele na nadhani ilikuwa kadi nyekundu."

Naye meneja wa Liverpool Kenny Dalglish: "Hatukucheza kama kawaida yetu lakini tulifanya juhudi kubwa angalao kupata chochote katika mchezo huu.

"Lakini hatujilaumu sana. Hata wakati tulipokuwa tukicheza 10 tuliendelea kutoa upinzani.

"Jay Spearing aliwania mpira, lakini alimchukiza mwamuzi baadae kwa kuinua juu miguu yake. Wakati mwengine ni kadi nyekundu, lakini kuna wakati si kadi nyekundu."