Golola bingwa wa ngumi na mateke

Nagy na Golola
Image caption Golola (kulia) akimtandika teke mpinzani wake

Moses Golola, mwanamichezo wa kickboxing wa Uganda, usiku wa Ijumaa aliweza kumtandika mpinzani Andras Nagy kutoka Hungary, na kutangazwa mshindi wa mkanda wa kimataifa wa WFK, uzani wa super middle.

Pambano hilo lilikwisha kwa utata.

Golola alikabidhiwa mkanda huo baada ya kukwaruzana vibaya mno na Andras Nagy katika raundi tano mjini Kampala.

Aliyealikwa kusimamia pambano hilo, Roger Mugisha, alimtangaza mwanamichezo tofauti kuwa mshindi, huku naye mwamuzi akiwa na jina tofauti.

Mugisha alisoma matokeo ya waamuzi, ambao wote kwa pamoja walikubaliana Golola ndiye mshindi.

Waamuzi wote watatu, kila mmoja alikubaliana kwamba Golola ni mshindi kwa 49-46.

Lakini mara tu baada ya Mugisha kutangaza hayo, mwamuzi Fritz Exenberger alibakura kijikaratasi hicho cha matokeo, na baada ya kuchukua kipaaza sauti, akasema kwamba matokeo hayo yalikuwa na dosari, na mshindi ni Nagy.

Waandishi wa habari hawakuweza kuona matokeo hayo, kwani Exenberger kwa haraka aliyarudisha ndani ya bahasha.