Man United yaua, Newcastle yayumba

Wayne Rooney na Nani wote walifunga mabao mawili kila mmoja wakati Manchester United ilipojisahihisha baada ya kutolewa katika heka heka za Ubingwa wa Ulaya kwa ushindi mzuri dhidi ya Wolves wa mabao 4-1.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nani akishangilia moja ya mabao yake

Nani alikuwa wa kwanza kuipatia Manchester United bao la kuongoza kwa mkwaju kutoka upande wa kushoto kabla hajafunga bao la pili kwa mkwaju wa chini chini.

Steven Fletcher aliirejeshea Wolves uhai baada ya kufunga bao moja kwa kichwa muda mchache kabla ya mapumziko.

Lakini Manchester United walijiuliza kipindi cha pili pale Antonio Valencia alipomtengea mpira Nani na kuachia mkwaju uliozaa bao la tatu na baadae Rooneya akaandika bao la nne.

Manchester United walisahau machungu ya kutolewa katika kinyang'anyiro cha Ubingwa wa Ulaya walipotolewa na Basel kwa kuonyesha soka maridadi ya kushambulia kwa kasi.

Robin van Persie alipachika bao pekee maridadi kwa mkwaju mkali wakati Arsenal ilipokuwa ikiadhimisha miaka 125 tangu iundwe na kuilaza Everton hali iliyoipandisha hadi nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu ya Soka ya England.

Van Persie kwa bao hilo amefikisha mabao 33 kwa msimu akiwa nyuma ya rekodi ya Alan Sheare ambaye alifunga mabao 36 kwa msimu mmoja.

Ilikuwa ni nafasi pekee ambayo Van Persie aliitumia kupachika bao ambapo awali Theo Walcott, Gervinho na Aaron Ramsey walipoteza nafasi nzuri za kufunga dakika za mwanzo.

Everton walikaribia kusawazisha lakini walipata nafasi moja tu ya mkwaju uliokwenda sawa langoni katika mchezo wote.

Kwa matokeo hayo Arsenal imeipiku Chelsea ambayo itapambana na Manchester City siku ya Jumatatu.

Luis Suarez aliifungia bao pekee Liverpool na kumaliza adha ya sare nne za nyumbani kwa klabu hiyo.

QPR waliidhibiti vilivyo Liverpool hadi sekunde ya 69 kipindi cha pili ambapo Suarez aliachwa bila kukabwa na akapachika bao kutokana na krosi aliyotengewa na Charlie Adam.

Liverpool walishindwa kuongeza bao la pili wakati mlinda mlango wa QPR alipookoa vizuri mkwaju wa Maxi Rodriguez.

QPR walikuwa wakitishia zaidi kwa mipira ya kona, lakini dakika za mwisho Shaun Wright-Phillips karibu angejifunga wakati akiwa katika heka heka za kuokoa na mpira ukagonga mwamba.

Grant Holt wa Norwich alifunga mabao mawili kwa kichwa wakati Newcastle inayokabiliwa na majeruhi wengi ikiteleza katika mchezo wake wa tatu wa ligi.

Norwich waliongoza wakati jitahada za Wes Hoolahan zilipozaa matunda lakini Demba Ba alisawazisha.

Wakiutumia vizuri uwanja wa nyumbani Norwich walifunga mara mbili katika kipindi cha pili kwa mabao ya kichwa ya Holt na Steve Morison.

Dan Gosling wa Newcastle alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Russell Martin, lakini Ba aliipatia Newcastle na kupunguza angalao deni, lakini alikuwa Holt aliyemaliza kazi kwa kufunga bao la nne.

Swansea City ilipata ushindi kwa urahisi kwa kuilaza Fulham mabao 2-0 yaliyofungwa na Scott Sinclair na Danny Graham katika kipindi cha pili.

Lakini mlinda mlango Michel Vorm wa Swansea alifanya kazi nzuri kwa kusiaidia timu yake kupata ushindi huo wa kwanza katika michezo mitano iliyopita kwa kuokoa mkwaju wa penalti wa Clint Dempsey.

Sinclair alikuwa wa kwanza kuipatia Swansea baada ya mkwaju wake kumgonga Dempsey na kujaa wavuni.

Vorm aliokoa mkwaju huo wa penalti kabla ya Danny Graham kupachika bao la pili katika dakika za nyongeza.

Wigan Athletic ikiwa imeshafungwa bao moja ilijirekebisha na kuilaza West Bromwich Albion na kujinasua kutoka eneo hatari la kushuka daraja.

Walikuwa ni West Brom walioanza kupachika bao wakati Steven Reid alipoachia mkwaju mkali wa adhabu ndogo ya moja kwa moja, lakini Victor Moses alisawazsiha kwa mkwaju wa yadi 12 baadae kidogo.

Ushindi huo wa Wigan ulitokana na mkwaju wa penalti uliopigwa na Jordi Gomez baada ya Reid kumchezea rafu Moses ndani ya sanduku la hatari.

Na mabao yaliyopachikwa na Marc Albrighton na Stiliyan Petrov yalitosha kuirejesha Aston Villa njiani kwenye uwanja wa Reebok, na kuzidisha machungu kwa Bolton wanaoendelea kuburura mkia.

Ivan Klasnic alifanikiwa kuipatia Bolton bao lakini dakika nazo zilikuwa zimeshawatupa mkono.

Ushindi huo umeisogeza Aston Villa hadi nafasi ya nane, huku Bolton wakiwa chini kabisa ya msimamo wa Ligi.