Khan ashtushwa na kipigo cha Peterson

Amir Khan amehuzunishwa na kushtushwa baada ya kushindwa kwa pointi na Lamont Peterson na kupoteza mikanda yake ya WBA na IBF - kwa uzito wa welterweight katika pambano la piga nikupige lilifofanyika Washington DC.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Raundi ya kwanza Khan alipomuangusha Peterson

Pointi mbili alizokatwa Khan kwa kusukuma ziliathiri matokeo yake baada ya majaji kutoa uamuzi wa 113-112, 113-112, 111-114 kwa Peterson.

Khan alimuangusha Peterson katika raundi ya kwanza, lakini Mmarekani huyo alijibu kwa makonde makali katika raundi ya tatu na ya saba.

Khan alimudu kusimama imara lakini baada ya kukatwa pointi nyingine kwa mara ya pili raundi ya mwisho ilitosha kummaliza.

"Ilikuwa kama napambana na watu wawili ulingoni - mwamuzi na Lamont mwenyewe," alilalamika Khan mara tu baada ya mshindi kutangazwa.

"Kila mara alipokuwa akinifuata alikuwa anainamisha kichwa chake chini. Mimi ni bondia ninayepigana kwa kufuata sheria, alikuwa amepanda mori sana ulingoni.

"Nilimsukuma kwa sababu kichwa chake kilikuwa chini wakati akinikabili."

Akizungumza kabla ya mpambano Khan mwenye umri wa miaka 25 alionesha nia ya kupanda uzito hadi uzani wa welterweight, huku bondia huyo anayeishi Bolton alivunjika moyo baada ya jaribio lake kufutika la kupigana pambano la kuunganisha mikanda ya uzito wa light-welterweight dhidi ya bingwa wa WBC Timothy Bradley na anayeshikilia taji la ubingwa wa WBO Erik Morales.

Khan ambaye aliwahi kunyakua medali ya fedha ya michezo ya Olimpiki alizungumzia hamu yake ya kuzichapa na Floyd Mayweather laikini matumaini yote hayo yanaonekana kuyeyuka baada ya kunyukwa na Peterson.

Peterson, baada ya pambano hilo alisema: "Sikupewa nafasi ya kushinda - watu wengi walidhani Khan atashinda.

Aliendelea kujigamba:"Bila shaka nitampa nafasi ya pambano la marudiano - alinipa nafasi ya kupambana naye kuwania ubingwa wa dunia, kwa nini nisirudiane naye? Lilikuwa pambano zuri, ninahakika kila mtu alifurahia na sitojali kupigana naye tena."