Redknapp hana nia kufundisha England

Meneja wa Tottenham Harry Redknapp hana nia ya kuchukua nafasi ya umeneja wa timu ya taifa ya England "kwa wakati huu", kwa mujibu wa mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Harry Redknapp hana tamaa kuifundisha England

"Harry bado ana miezi 18 kabla mkataba wake haujamalizika. Kwa ninavyomfahamu Harry, hana tatizo hapa na hataki hata kufikiria kwa wakati huu kazi ya kuifundisha England," alisema Levy.

"Tutakuwa na wasiwasi iwapo suala hili litajitokeza wakati wa msimu ujao wa usajili."

Meneja wa sasa wa England Fabio Capello atamaliza mkataba wake mwishoni mwa fainali za michuano ya Euro mwaka 2012.

Redknapp awali aliwahi kusema kazi ya umeneja wa England "itakuwa vigumu kuikataa" na kuielezea kazi hiyo kama ni "lulu kwa atakayeipata".

Redknapp mwenye umri wa miaka 64 alichukua hatamu za kuifundisha Tottenham mwezi wa Oktoba mwaka 2008 wakati huo timu hiyo ikiwa na pointi nne kutoka eneo la kushuka daraja kwa msimamo wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England baada ya kuwa na wakati mgumu mwanzoni walipokuwa chini ya meneja kutoka Hispania Juande Ramos.

Amejitahidi kuinyanyua Spurs hadi kuweza kucheza michuano ya Ubingwa wa Ulaya msimu wa 2009-10.

Wakati huo huo meneja huyo wa Tottenham ameonywa achunge kauli zake siku zijazo kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Chris Foy walipofungwa na Stoke.

Redknapp alisema alikuwa na wasiwasi Foy "alikuwa akifurahia kutotupatia chochote" walipolazwa mabao 2-1.