Dede Ayew ashinda tuzo ya BBC

Dede Andre Ayew
Image caption Dede Andre Ayew

Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Ghana, Black stars na klabu ya nchini Ufaransa,Marseille, Andre 'Dede' Ayew ameshinda shindano la mcheza soka bora wa Afrika mwaka 2011 linaloandaliwa na BBC.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 21 alishinda kwa theluthi ya kura zote zilizopigwa na wasikilizaji na hivyo akifuata nyayo za babake Abedi Pele Ayew aliyeshinda shindano hilo mnamo mwaka 1992. Ayew alifuatiwa na Yaya Toure wa Ivory Coast na klabu ya Manchester City kwa karibu na pia mchezaji mwingine wa Ivory Coast, Gervinho, Samuel Eto'o wa Cameroon na Seydou Keita kutoka Mali walishindwa. Andre Ayew aliweza kufunga jumla ya mabao 12 katika mechi 22 kwa klabu yake ya Marseille msimu huu.

Shindano hili lilishirikisha wasikilizaji wa matangazo ya BBC waliomchagua mchezaji waliyemdhania kua anastahili kushinda kupitia ujumbe wa simu ya kiganjani na barua pepe'' au email.

Wasikilizaji walifuatia orodha ya wachezaji waliotajwa baada ya kupendekezwa na kamati ya wataalamu wa soka kutoka takriban kila nchi barani Afrika, wakichagua wachezaji kwa kutegemea uwezo wao, uchezaji, umahiri wa kuelewa mchezo, ushirikiano uwanjani na nidhamu.

Baada ya kuonekana mnamo mwaka 2010, alipowavutia wadadisi wengi kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika pamoja na Kombe la Dunia la mwaka 2010. Mwaka 2011 ndiyo mwaka ambapo Ayew alizidi kushamiri kwa ngazi ya klabu.

Alimaliza msimu wa mwaka 2010-2011 akishiriki kila mechi ya Marseille kwa mara ya kwanza akifunga jumla ya mabao 11.

Mwanzoni mwa msimu huu aliweza kufunga mara tatu katika mechi moja na kuiwezesha klabu ya Marseille kushinda Ligi kuu ya Ufaransa, na tangu hapo ameweza kushiriki mechi 17 za klabu hio akifunga mara sita.

Tangu alipokwamishwa na majeruhi yaliyomkosesha mechi ya ufunguzi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, kijana huyo amekosa dakika moja tu ya mashindano hayo ya Ulaya pale mabingwa hao wa Ulaya wa mwaka 1993 walipoingia hatua ya mtoano.

Kwenye medani ya kimataifa, Ayew alitoa mchango mkubwa katika kuhakikisha kua Black Stars ya Ghana inafuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012 bila kupoteza mechi hata moja.

Mnamo mwaka 1992, Abedi 'Pele' Ayew alijitokeza kua mshindi wa mwanamichezo bora wa shindano la BBC ambalo baadaye shindano likageuka kua shindano la mcheza soka bora wa BBC.

'dede Ayew ni raia wa tano kutoka Ghana kushinda shindano hilo akifuata nyayo za babake Abedi Pele. Baada ya Pele alifuata Samuel Kuffuor (2001), Michael Essien (2006) na mwaka jana alikua Asamoah Gyan.