NDOTO ZA OLIMPIKI KATIKA PICHA

Imebadilishwa: 14 Januari, 2012 - Saa 15:55 GMT

Ndoto za Olimpiki

 • Usain Bolt, mwanariadha kutoka Jamaica na anatazamiwa kufanya maajabu 2012

  "Mimi sio 'mkongwe' bado. Naelekea huko, lakini nahitaji kwenda London na kuwafurahisha watu."

  Usain Bolt ni mmoja wa wanariadha machachari duniani ambaye anafuatiliwa kwa karibu na BBC wakatiwakijiandaa na michuano ya Olimpiki ya London 2012. Je wamefanikiwa kiasi gani mwaka 2011? Ushindi wa kishindo sio kitu ambacho Usain Bolt atasema atajivunia mwaka 2011. Alitolewa katika fainali ya mita 100 ya michuano ya dunia kwa kuanza kabla ya wenzake. Hata hivyo alitetea ubingwa wake wa mita 200 na kuweka rekodi mpya na timu ya mbio za vijiti za mita 4x100. Alimaliza msimu kwa muda wake wa kasi katika mita 100 kwa sekunde 9.6 mjini brussels, Ubelgiji.

 • Nadel el Masri, mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Gaza na anatarajia kushiriki Olimpiki Lomdon 2012

  "Nina kocha lakini hakuna aliye kwenye kiwango changu Gaza. Nalazimika kufanya mazoezi yangu peke yangu"

  Nadel el Masri, mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Gaza na anatarajia kushiriki Olimpiki Lomdon 2012

  El Masri alithibitishwa kuwa ni mwanariadha mahiri, wakati aliposhinda mbio za kwanza kuwahi kufanyika Gaza. Mpalestina huyo amekimbia muda wake mzuri wa dakika 14 na sekunde 21 katika mita 5,000 - wakati muda wa kufuzu Olimpiki ni dakika kumi na tatu na sekunde 27. El Masri ameambiwa hatopewa nafasi ya kufuzu bila kufikia kiwango katika michuano ya 2012.

 • Alistair Brownlee, Mwingereza Bingwa mara mbili wa dunia wa triathlon na anatarajiwa kushiriki Olimpiki London 2012

  "Ilikuwa kweli, kweli siku muhimu kwangu kuwa bingwa wa dunia mara mbili! si watu wengi wanaweza kusema hivyo"

  Alistair Brownlee, Mwingereza Bingwa mara mbili wa dunia wa triathlon na anatarajiwa kushiriki Olimpiki London 2012

  Alistair alivishwa taji la dunia mwezi Septemba, na kuongeza taji la dunia aliloshinda mwaka 2009. alimaliza mwaka wake vyema baada ya kutetea ubingwa wa Ulaya nchini Uhispania na pia kufuzu michuano ya London 2012 baada ya kushinda michuano ya Hyde Park triathlon.

 • Haider Rashid, mpiga makasia kutoka Iraq na mtarajiwa katika michuano ya Olimpiki ya London 2012

  "Nitafanya kila niwezavyo kufuzu kwa sababu nahitaji kufanya hivyo"

  Haider Rashid, mpiga makasia kutoka Iraq na mtarajiwa katika michuano ya Olimpiki ya London 2012

  Haider Rashid alimwambia Matthew Pinsent katika michuano ya dunia ya kupiga makasia nchini Slovenia kuwa lengo lake kwa mwaka 2011 ni kufuzu kushiriki Olimpiki ya London 2012. Rashid alimaliza katika nafasi ya 27 kati ya washiriki 34 upande wa wanaume, na bado ana nafasi ya kufuzu kupitia mchujo wa Asia utakaofanyika Aprili 2012.

 • Olga Kharlan, mcheza fensi wa Olimpiki kutoka Ukraine

  "Bibi yangu anasema tayari nina kila kitu ambacho wao hawakuwahi kuwa nacho maisha yao yote"

  Olga Kharlan, mcheza fensi wa Olimpiki kutoka Ukraine

  Ulikuwa mwaka ambao Olga alitawala Ulaya na almanusura atawale dunia. Alishinda ubingwa wa Ulaya mjini Sheffield lakini aliambulia medali ya shaba katika michuano ya dunia nchini Italia. Kibinafsi, ameshinda na kupata kipato cha kujenga nyumba yake na kuweza kuhama katika nyumba ndogo ya wazazi wake.

 • Julien Absalon, mwendesha baiskeli wa Ufaransa na mtarajiwa wa Olimpiki London 2012

  Julien Absalon, mwendesha baiskeli wa Ufaransa na mtarajiwa wa Olimpiki London 2012

  Mfaransa huyu mara nyingi hutawala michuani ya nyika ya dunia lakini mwaka 2011 alifanikiwa tu kupata mdedali ya fedha katika michuano ya Ulaya na shaba katika michuano ya dunia. Hata hivyo ametawazwa kuwa bingwa wa Ufaransa kwa mara ya tisa na pia alishinda michuano ya London Olympic Test 2012 iliyofanyika Hadleigh Farm, Essex nchini Uingereza.

 • Majlinda Kelmendi, mcheza judo kutoka Kosovo na mtarajiwa katika michuano ya Olimpiki ya London 2012

  "Nimekataa wito kutoka nchi kadhaa kubwa, lakini naiwakilisha Kosovo na sitaki mtu aniambie kwamba haiwezekani"

  Majlinda Kelmendi, mcheza judo kutoka Kosovo na mtarajiwa katika michuano ya Olimpiki ya London 2012

  Kufuzu kushiriki London 2012 kulihakikishwa mwezi Oktoba wakati Majlinda aliponyakua medali tatu za dhahabu katika muwa wa wiki tatu. Mafanikio yake yalimpandisha hadi katika nafasi ya tatu katika msimamo wa dunia wa mchezo wa judo katika utizo wa kilo 52. Mwaka 2012 Majlinda ana matumaini ya kuwa mwanamichezo wa kwanza kuiwakilisha Kosovo katika Olimpiki - jambo gumu ukizingatia nchi hiyo haitambuliwi rasmi ya Kamati yya Olimpiki ya Kimataifa IOC.

 • Jehue Gordon, mwanariadha kuruka viunzi kutoka Trinidad na mtarajiwa katika michuano ya Olimpiki ya London 2012

  "Hauhitaji kujizuia kutokana na hali uliyonayo. Kwa sababu unatokea geto haimaanishi uwe na tabia za kigeto."

  Jehue Gordon, mwanariadha kuruka viunzi kutoka Trinidad na mtarajiwa katika michuano ya Olimpiki ya London 2012

  Katika mbio za Diamond League mwezi Mey, Jehue alikimbia kwa muda wa sekunde 49.09, muda wa kutosha wa kufuzu kushiriki Olimpiki ya London. Alisikitika wakati aliposhindwa kufuzu kukimbia fainali ya mita 400 katika michuano ya dunia kwa kukosa moja ya mia moja ya sekunde. Wiki moja na nusu baadaye aliweka muda mzuri binafsi wa sekunde 48.66 - muda wa kasi wa 13 mwaka 2011.

 • Linet Masai, mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Kenya na mtarajiwa wa Olimpiki London 2012

  Linet Masai, mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Kenya na mtarajiwa wa Olimpiki London 2012

  Linet alianza mwaka kwa kushinda mbio za Great Winter mjini Edinburgh, Scotland. Alimaliza sekunde nane mbele ya mwenzake Vivian Cheruiyot, ambaye alilipiza kisasi kwa kumshinda katika michuano ya dunia ya nyika - kwa mara ya tatu mfululizo Linet alimaliza wa pili. Aliweza kutetea taji lake la New York la kilomita 10, lakini katika michuano ya dunia ya Korea, alishindwa na Vivian Cheruiyot ambaye alinyakua taji la Linet la mita 10,000.

 • Luol Deng, mchezaji wa mpira wa kikapu kutoka Uingereza na mtarajiwa wa michuano ya Olimpiki ya London 2012

  "Nimefurahi sana kuwa tuko wote hapa, kila mtu aliyekimbia. Nimefurahi kuwa hata wazazi wangu wameweza kushuhudia siku hii ya leo. Kila walichojitolea kimetufaa."

  Luol Deng, mchezaji wa mpira wa kikapu kutoka Uingereza na mtarajiwa wa michuano ya Olimpiki ya London 2012

  Luol Deng atashiriki katika michuano ya London 2012 baada ya Fiba, shirikisho la mchezo huo la dunia, kuipa timu ya Uingereza ruhusa ya kushiriki.Na baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa kimataifa wa mwaka na chama cha waandishi wa habari wa Uingereza, Luol Deng alikuwa alikuwa mchezaji nyota wa timu ya Uingereza katika michuano ya Ulaya ya mpira wa kikapu. Mbali na michezo, Luol pia alizuru Sudan Kusini kwa mara ya kwanza tangu alipokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati wakiwa mtoto.

 • MC Mary Kom, bondia wa India na mtarajiwa wa michuano ya Olimpiki ya London

  "Ulikuwa uamuzi wa mgumu kwake kuondoka kabla ya upasuaji wa mtoto wetu wa kiume, lakini aliniahidi kuwa atachukua nafasi ya kwanza, na nimefurahi alifanya hivyo." Omler Kom

  MC Mary Kom, bondia wa India na mtarajiwa wa michuano ya Olimpiki ya London

  Bondia huyo mwenye mwili mdogo kutoka Manipur amelazimika kuganwanya muda wake kufanya mazoezi na kuhmhudumia mwanaye mmoja ambaye ni mgonjwa. Wakati mwanae anaandaliwa kupelekwa kufanyiwa upasuaji wa moyo, Mary Kom alinyakua kombe la Asia kabla ya kushinda taji la nane la ubingwa wa India katika kipindi cha miaka 12. Mwezi Novemba alihudhuria majaribio ya Olimpiki na kuzua utata kuhusu mabondia wa kike kwa kusema wanalazimishwa kuvaa sketi, akisema: "Wacheza tennis wanavaa sketi, wacheza badminton wanavaa sketi, kwa nini mabondia wasivae pia sketi?"

 • Merlin Diamond, mkimbiaji kutoka Namibia na mtarajiwa katika michuano ya Olimpiki ya London 2012

  "Ukitafuta maisha mazuri na unataka kupata mazuri kutokana na unachofanya, inabidi utoke na ujitolee katika mambo mengi."

  Merlin Diamond, mkimbiaji kutoka Namibia na mtarajiwa katika michuano ya Olimpiki ya London 2012

  Mwaka 2011 kwa Merlin Diamond haukuwa wenye mn'garo sana. Mwanzo mwa mwaka alikwenda Uingereza kwa mara ya kwanza kuutazama uwanja wa Olympic Park mashariki mwa London. Baadaye aliwaacha ndugu zake na marafiki na kuhudhuria mazoezi ya hali ya juu katika kisiwa cha Mauritius. Ingawa alikuwa na bahati kwa kudhaminiwa na IOC, vifaa vilikuwa duni na akapatwa na msongo wa mawazo. Aliporejea Namibia alikuwa amenenepa na akishindwa hata kukimbia na kuweza kufuzu London 2012.

 • Rohullah Nikpai, mchezaji wa taekwondo kutoka Afghanistan na mtarajiwa wa michuano ya Olimpiki ya London 2012

  "Kupitia kushinda medali nina imani ya kuleta amani na maelewano katika nchi"

  Rohullah Nikpai, mchezaji wa taekwondo kutoka Afghanistan na mtarajiwa wa michuano ya Olimpiki ya London 2012

  Mshindi pekee wa medali ya Olimpiki kutoka Afghanistan yuko tayari kusaka medali nyingine 2012. Rohullah alifuzu kushiriki London 2012 kwa kunyakua medali ya shaba katika uzito wa kilo 68 katika michuano ya kufuzu ya Olimpiki mjini Bangkok, Thailand. Hii ilifuatiwa na medali ya shaba aliyoshinda mwezi Mei katika michuano ya dunia ya taekwondo nchini Korea Kusini.

 • Shawn Johnson, mwanasarakasi kutoka Marekani na mtarajiwa wa michuano ya Olimpiki ya London 2012

  "Mimi kuchaguliwa, ilisababisha nikatoa machozi. Kurejea katika timu ni jambo muhimu kwangu. Nilikuwa nikisema, ni majaribio tu, lakini sasa imekuwa kweli."

  Shawn Johnson, mwanasarakasi kutoka Marekani na mtarajiwa wa michuano ya Olimpiki ya London 2012

  Baada ya kuumia goti katika ajali ya mchezo wa kuteleza kwenye barafu mwaka 2010, Shawn Johnson alipigana kufa na kupona kurejea katika timu ya sarakasi wa Marekani mwaka 2011. kwa bahati mbaya hakuchaguliwa katika michuano ya dunia ya sarakasi mjini Tokyo. Badala yake, alishinda medali mbili katika michuano ya Pan American. Kampuni ya Nike ilionesha imani yake kwa mwanamichezo huyo kwa kumpa udhamini na sasa ana hadi mwezi Juni kujiandaa kwa ajili ya timu ya Marekani ya Olimpiki katika majaribio mjini San Jose.

 • Wu Minxia, mchupaji kutoka Uchina na mtarajiwa wa Michuano ya Olimpiki ya London 2012

  "Mimi ndio msichana mwenye umri mkubwa zaidi katika timu, kwa hiyo nina majukumu kama ya dada na timu yote wananiita dada Xia."

  Wu Minxia, mchupaji kutoka Uchina na mtarajiwa wa Michuano ya Olimpiki ya London 2012

  Wu Minxia na mchupaji mwenzake He Zi walishinda mara nne michuano ya dunia kabla ya kufuzu kucheza London 2012. Kila walichofanya kiliwapatia dhahabu na walitawala michuano ya dunia mjini Shanghai kwa mara ya kwanza wakicheza pamoja. Hata hivyo ilikuwa ni dhahabu ya michuano ya kuchupa majini nchini Uhcina mwezi Septemba ndio iliwapatia nafasi ya kufuzu kwa ajili ya michuano ya London. Tangu 'malkia wa kuchupa' Guo Jingjing alipostaafu, Wu amekuwa ndio kinara wa Uchina katika kuchupa, chama cha kuogelea kilimtunuku tuzo ya mchupaji bora wa kike wa mwaka.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.