Sunderland yaishangaza Man City

Ji Dong-won Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ji aliiwezesha Sunderland kuishinda

Bao la Ji Dong-won katika muda wa majeruhi siku ya Jumapili uliiwezesha Sunderland, ikicheza nyumbani kupata ushindi ambao uliwashangaza mashabiki wa Manchester City, ambao hadi sasa wanaongoza ligi kuu ya Premier.

City walikuwa na matumaini kwamba kwa Manchester United kushindwa na Blackburn siku ya Jumamosi, walikuwa na nafasi nzuri ya kuongeza tofauti ya pointi kati yao na mahasimu wao jirani.

Lakini kama meneja Martin O'Neill alivyokuwa amemueleza mwandishi wetu Peter Musembi wiki iliyopita, Sunderland ilitazamia kuonyesha mchezo wa kuburudisha, katika kile alichokuwa amekielezea kama mchezo 'fantastic'.

Kutokana na Nicklas Bendtner na Stephane Sessegnon kukosa kufunga hapo awali katika kipindi cha kwanza na vile vile kipindi cha pili, wakati Edin Dzeko na Micah Richards walikosa mabao, ilielekea ushindi ulikuwa wa Sunderland, kwani Ji aliweza kumzunguka mlinda lango Joe Hart na kuutambariza mpira wavuni.

Ilikuwa ni mechi ya kusisimua, licha ya baadhi ya mashabiki kuhisi kwamba mchezaji huyo wa Korea alipata bao hilo kwa kuotea, alipoupokea mpira kutoka kwa Sessegnon.

Hata hivyo, makocha wengi bila shaka wangelifurahia kuwa na timu ambayo inaweza kufanya juhudi kubwa katika kulinda lango, kama walivyofanya Sunderland, licha ya nyakati fulani ngome yao kuoenekana kuwa dhaifu.

Ushindi huo sasa umemwezesha meneja mpya O'Neill kupata ushindi wake wa tatu, kati ya mechi tano, tangu alipochukua madaraka katika uwanja huo wa Stadium of Light, na Sunderland sasa imo katika nafasi ya 13 katika ligi kuu ya Premier.

Watangazaji wa Ulimwengu wa Soka Charles Hilary na Salim Kikeke, kwa mara ya kwanza walitangaza wakiwa uwanja wa Stadium of Light.