Dalglish atetea msimamo wao kwa Suarez

Kenny Dalglish ametetea utaratibu uliotumiwa na Liverpool wakati wa kushughulikia shauri la Luis Suarez na amesisitiza ukweli wote kuhusiana na suala hilo haujawekwa bayana.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Dalglish atetea uamuzi wa Liverpool kwa Suarez

Liverpool haitakata rufaa dhidi ya adhabu ya kufungiwa mechi nane kwa Suarez kwa kumtusi maneno ya kibaguzi mlinzi wa Manchester United Patrice Evra.

Lakini Suarez mwenyewe na klabu wamesema hawana hatia katika taarifa kali waliyoitoa.

Tume huru ya Chama cha Soka cha England ilitoa uamuzi kwamba Suarez, mwenye umri wa miaka 24, alimtusi kwa maneno ya kibaguzi Evra wakati Liverpool na Manchester United zilipotoka sare ya bao 1-1 mwezi wa Oktoba.

Ripoti iliyotolewa na tume hiyo imesema Suarez, alitumia neno "negro" mara saba katika muda wa dakika mbili na imedai kitendo hicho kimeharibu hadhi ya kandanda ya Uingereza duniani.

Pia tume hiyo ilimshutumu mshambuliaji huyo kwa kutoa ushahidi "usioaminika na" "usio imara" wakati wa kusikiliza shauri lake.

Liverpool ilitangaza haitakata rufaa dhidi ya kufungiwa kwa Suarez na lakini bado mchezaji mwenyewe pamoja na klabu wametoa taarifa ambapo wamepinga kubebeshwa lawama na kushutumu namna suala hilo lilivyoendeshwa.

Katika taarifa yake, Suarez alisema: "Nitaendelea kutumikia adhabu huku nikijua kuna mtu hajafanya kosa lolote ambaye pia anahisi amehuzunishwa kutokana na utukio lenyewe."

Baada ya Liverpool kupokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Manchester City, ambapo Suarez hakucheza akiwa ameanza kutumikia adhabu yake, Dalglish alisema: "Luis ametoa taarifa nzuri sana na tunamuunga mkono.

Suarez alikiri kutamka neno "negro" dhidi ya Evra, lakini Dalglish aliitaka tume hiyo huru ingetilia maanani historia na uraia wa mshambuliaji huyo anayechezea pia timu ya taifa ya Uruguay.

Na Dalglish ametetea kwa nguvu uamuzi wake na wachezaji wake walipovaa fulana kwa kumuunga Suarez walipocheza na Wigan kabla ya Krismasi.