Netiboli kutimua vumbi Zanzibar

Zanzibar
Image caption Michuano ya Nnetiboli kwa ajili ya miaka 48 ya mapinduzi

Timu za mataifa kadhaa ya Afrika Mashariki na Kati kwa mchezo wa netiboli zinaingia katika mtifuano wa Kombe la Mapinduzi Visiwani Zanzibar katika michuano ambayo itafanyika kwenye Kiwanja cha Gymkhana na kuanza Ijumaa.

Kwa mujibu wa Sherry Khamis, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Zanzibar michuano hiyo itafikia hatima yake Januari 12, siku ambayo ni kilele cha Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yanatimiza miaka 48.

Sherry, aliye afisa wa Shirika la Netboli la Afrika na mwana netiboli wa timu ya taifa amesema nchi ambazo zitashiriki ngarambe hiyo ni pamoja na za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania. Lakini pia kutakuwa na nchi za Zimbabwe, Zambia na huku pia ikitarajiwa Msumbiji ambao ni wageni katika mchezo huo wa netboli na wao watatia timu hapa Zanzibar.

Michuano hiyo itakuwa ni kwa wanaume na wanawake lakini ni timu za Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania ndio zilizothibitisha kuleta Zanzibar timu za wanaume kwa kuwa upande wao utakuwa umeshstawi katika nchi hizo.

Michuano hiyo ni muhimu kwa nchi za kanda hii kwa vile zitasaidia katika mayarisho ya michuano mikubwa iliyo mbele pamoja na mtoano kulekea Olimpiki ya London baadae mwaka huu.

Mwandishi wetu wa Zanzibar Ally Saleh anasema hamu ya mashindano hayo imepanda huko Zanzibar ambapo mchezo wa netboli unapendwa sana baada ya mpira wa miguu na mpira wa kikapu.

Kwa Tanzania mashindano hayo ni kielelezo muhimu kwa Tanzania ambayo ilishinda medali katika michuano ya Nchi za Kiafrika iliyofanyika Msumbiji mwezi ujao.

Pia michuano hio itaisaidia Tanzania kutibu majeraha ya mivutano ya muda mrefu baina ya vyama vya netiboli vya Zanzibar na Tanzania Bara kwa kuweza kuunda timu ya taifa itayoweza kuleta ushindani na kuipa Tanzania jina inalostahili katika mchezo huo.