Suarez aomba radhi kwa sakata la ubaguzi

Mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez ameomba radhi kijumla baada ya kuadhibiwa kutocheza mechi nane kwa kumtolea maneno ya karaha ya kibaguzi Patrice Evra.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Luis Suarez aomba radhi kwa matamshi yake ya kibaguzi

Suarez hajamuomba radhi moja kwa moja mlinzi huyo wa Manchester United ambaye alipatikana na hatia kwa kumuita "negro".

Amesema: "Nilikiri mbele ya tume nilitamka neno hilo kwa lugha ya Kihispania mara moja, mara moja tu.

"Kamwe sijawahi kutumia neno hilo kwa nia ya kuvunja heshima na kama kuna mtu yeyote anahisi nimemkwaza kutokana na kutumia neno hilo naomba radhi kwa hilo."

Ameongeza: "Niliwaambia wajumbe wa tume kwamba sitatumia tena neno hilo nikiwa uwanjani nikisakata kandanda nchini England."

Tume huru ya Chama cha Kandanda cha England kiliamua Suarez, mwenye umri wa miaka 24, alimtukana kwa kutumia maneno ya kibaguzi Evra wakati Liverpool ilipotoka sare ya bao 1-1 na Manchester United mwezi wa Oktoba.

Tume hiyo imesema Suarez alitumia neno "negro" mara saba katika muda wa dakika mbili na imedai amevunjia heshima kandanda ya Uingereza duniani kote kutokana na tabia yake hiyo.

Pia tume hiyo ilimshutumu kwa kutoa ushahidi "usioaminika na "ulioyumba" wakati akijitetea.

Kwa kiasi kikubwa Suarez ameshutumiwa kwa kushindwa kumuomba radhi moja kwa moja Evra na mshambuliaji wa Blackburn Jason Roberts anaamini Suarez hana kutumia neno hilo.

"Kutumia neno hilo kwa sauti na muktadha uliokuwepo kamwe haukubaliki katika ligi yetu," Roberts aliiambia BBC.

"Haitoshi tu kusema ni sawa kutumia neno hilo huko ninakotoka, kwa hiyo basi na hapa unaweza tu'. Hiyo si njia sahihi ya kuieleza jamii yetu ama Ligi Kuu. Ilikuwa ni mbaya sana na nina wasiwasi watoto watakuwa wameona walivyokuwa wakilumbana."

Mkuu wa Chama cha Wacheza Kandanda wa Kulipwa Gordon Taylor alisema adhabu ya Suarez imetoa onyo kwamba ubaguzi katika kandanda hautavumiliwa.