Ferguson akanusha kumuwinda Lampard

Kiungo wa Chelsea Frank Lampard hatajiunga na Manchester United kwa mujibu wa meneja Sir Alex Ferguson.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Sir Alex Ferguson hana nia ya kumsajili Frank Lampard

Kulikuwa na uvumi Lampard huenda akajiunga na Manchester United lakini Ferguson hatarajii kumsajili katika dirisha hili dogo la usajili la mwezi wa Januari.

"Unaweza kupata nini mwezi wa Januari? Unafanya nini? Unachukua mchezaji wa kiwango cha chini? Hapana, bila shaka huchukui."

Manchester United imepoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu, walipolazwa na Blackburn nyumbani na baadae wakachabangwa na Newcastle nje, hali hiyo imesababisha kuwepo na hisia kwamba sehemu ya kiungo inahitaji kuimarishwa wakati huu Darren Fletcher na Tom Cleverley watakapokuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Lampard, ambaye ameshafunga mabao tisa msimu huu, alikiri wiki iliyopita kwamba anakatishwa tamaa katika klabu ya Chelsea ambapo ama huchezeshwa akiwa mchezaji wa akiba au hupumzishwa kupisha mchezaji mwengine mara 11 katika michezo 25 aliyocheza msimu.

Amebakisha miezi 18 katika mkataba wake lakini Ferguson akaongeza: "Huwezi kuniambia kama Chelsea watamuuza Frank Lampard kwa Manchester United mwezi wa Januari.

"Chelsea wapo kama sisi. Wanataka kufanya jambo fulani. Nusu ya pili ya msimu itakuwa muhimu kwetu.

"Iwapo wanataka kujaribu kushinda ligi basi watahitaji kuwa na wachezaji wao bora."

Ferguson anaamini ni vyema kuonesha imani kwa wachezaji alionao Old Trafford.