Thierry Henry ajiunga Arsenal kwa mkopo

Thierry Henry amejiunga na Arsenal kwa mkopo wa miezi miwili akitokea klabu ya New York Red Bulls.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Thierry Henry kuichezea Arsenal kwa miezi miwili kwa mkopo

Nahodha huyo wa zamani wa Arsenal ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 34, amekuwa akifanya mazoezi na wachezaji wa Arsenal wakati huu Ligi Kuu ya Marekani ikiwa mapumzikoni.

Mshambuliaji huyo ataichezea Arsenal kwa mwezi wa Januari na Februari, wakati huu Gervinho akielekea kuiwakilisha nchi yake ya Ivory Coast katika michezo ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Henry, ambaye sasa ataweza kuichezea Arsenal siku ya Jumatatu katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Leeds itakayochezwa uwanja wa Emirates, alisema: "Inapokuja suala la Arsenal moyo wangu kila mara unasisimka."

Mshambuliaji huyo alikuwa maarufu kwa fulana namba 14, ambayo kwa sasa inavaliwa na Theo Walcott . Henry kwa sasa atakabidhiwa fulana itakayokuwa na namba 12.

Meneja Arsene Wenger ameongeza: "Nina furaha sana. Nilikuwa natamani na pia Thierry mwenyewe alikuwa anatamani kujiunga.

"Tutakuwa na Thierry kwa mwezi wa Januari na Februari, baadae ataondoka kurejea Marekani.

"Nina hakika katika miezi hii miwili atatusaidia kwa kiwango kikubwa, kwenye chumba cha kuvalia na uwanjani.

"Hatakuwa katika chagizo kubwa sana ili aweze kutoa mchango wake kwa timu."