Amir Khan adai mchezo mchafu uliongoni

Amir Khan amemtuhumu mtu asiyejulikana kwa "kuwaingilia" majaji na maafisa wengine walipokuwa wakitoa pointi alipotwangwa na Lamont Peterson.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Amir Khan adai kushindwa kwake kulikuwa na mkono wa mtu

Khan ametoa malalamiko hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kuonesha picha kadha kutokana na mpambano wake wa mwezi uliopita mjini Washington.

Bondia huyo mwenye maskani yake Bolton amesema picha hizo zinaelezea wasiwasi wake kuhusu kuonekana mtu huyo nje ya ulingo.

Khan, amedai mtu huyo alizungumza na na msimamizi wa WBA Michael Welsh na aliingilia utoaji wa pointi uliokuwa ukifanywa na majaji.

Rufaa yake dhidi ya kushindwa kwa pointi kulikoonekana kulikuwa na utata alipopambana na Peterson, hali iliyosababisha apoteze mataji yake ya WBA na IBF kwa uzito wa light-welterweight, itasikilizwa baadae mwezi huu.

Rais wa WBA, Gilberto Mendoza, ameiambia BBC anachunguza madai ya Khan aliyoandika katika mtandao wa Twitter na ataijibu kambi ya Khan ndani ya kipindi cha saa 24.

Nayo IBF imeiambia BBC kwamba "kwa kuzingatia utaratibu wa kutoa pointi IBF wangependa kutoa uhakikisho hakuna mtu aliyeingilia utaratibu wa kutoa pointi".

Miongoni mwa mengi aliyoyaandika katika mtandao huo, Khan amedai mtu asiyejulikana alianza "kuingilia" katika raundi ya sita na akaendelea kufanya hivyo hadi mwisho wa pambano.

Pia alidai mtu huyo alizungumza naye na akampatia kadi yenye matokeo, ambayo alikuwa akipewa kila baada ya raundi na Khan amekiri baada ya pambano kwamba kadi yake ya pointi ilikuwa haioani na nyingine.

Mwezi uliopita Khan alieleza kutofurahishwa na namna mwamuzi Joe Cooper alivyokuwa akisimamia pambano hilo - ambaye alimkata pointi mbili kwa kosa la kusukuma - na kutoa madai ya kukiukwa kwa taratibu za utoaji matokeo.