Caf yasema Namibia kesi yao imetupwa

Shirikisho la Kandanda barani Afrika -Caf, limesema madai ya Namibia dhidi yake mbele ya mahakama ya rufaa za michezo, yametupiliwa mbali.

Image caption Caf yadai rufaa ya Namibia dhidi yake imetupwa

Iwapo hiyo itathibitika itakuwa basi Burkina Faso wataendelea kushikilia nafasi yao ya kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, inayoanza tarehe 21 mwezi wa Januari.

Chama cha Kandanda cha Namibia kimesema bado hakijaarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo na bado hakuna kilichochapishwa katika mtandao wa mahakama ya rufaa za michezo.

Namibia imedai kwamba Burkina Faso ilimtumia mchezaji asiyepaswa kucheza katika michezo ya kufuzu kwa Kombe hilo la Afrika na badala yake wao ndio wangeshiriki katika fainali hizo.

Rufaa yao kwa Caf juu ya kuchezeshwa Herve Zengue ilitupwa mara mbili, hali iliyosababisha shauri lao walipeleke mbele ya mahakama inayosikiliza mashauri ya michezo.