Man City na Milan bado wamzungumza Tevez

Manchester City imeanza mazungumzo na Inter Milan juu ya kumuuza mshambuliaji Carlos Tevez.

Haki miliki ya picha PA
Image caption City na Inter wajikita kuzungumzia usajili wa Tevez

City imekuwa na mazungumzo na klabu ya AC Milan lakini ilivunjika moyo baada ya mabingwa hao wa Italia kushikilia msimamo wa kutaka kumchukua kwa mkopo badala ya kumnunua moja kwa moja.

Wawakilishi wa Tevez bado hawajazungumza na Inter na hakuna ada waliyoafikiana kwa ajili ya Tevez.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina anapendelea kujiunga na AC Milan na washauri wake wanataka kulimaliza suala lake kabla ya dirisha la usajili halijafungwa.

Rais wa Inter Milan Massimo Moratti alisema siku ya Jumatatu: "Iwapo unahitaji kufanya jambo fulani hulifanyi kama ni mzaha lakini kwa sababu unahisi linaweza kuwa la manufaa.

"Tumepokea taarifa ya namna mambo yanavyokwenda, kuna nafasi ya kuingilia, tutaangalia kama tutafanikiwa au la.

"Kuna wiki tatu zimesalia. Si suala la kuwa na matumaini makubwa lakini zaidi ni kuangalia namna mambo yalivyo."

Inter Milan wanaoshikilia nafasi ya tano ya msimamo wa ligi ya Italia ikiwa nyuma kwa pointi 10 dhidi ya AC Milan, imekuwa na mwanzo mbaya msimu huu wa ligi na timu hizo zitapambana katika mchezo wa ligi mwishoni mwa wiki.

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini alisema ana matumaini Tevez atapata klabu mpya kabla ya kukamilika dirisha la usajili la mwezi wa Januari.

Tevez hajaichezea Manchester City tangu walipoilaza Birmingham tarehe 21 mwezi wa Septemba.