Steven Gerrard akwaruzana na Mancini

Mancini Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Roberto Mancini

Kocha wa klabu ya Manchester City Roberto Mancini alirushiana maneno makali na nahodha wa klabu ya Liverpool Steven Gerrard baada ya kupoteza pambano la Kombe la Carling 1-0.

Kocha huyo alihisi kua kosa la Glen Johnson la kumpinga ngwara Joleon Lescott lilistahili adhabu kwa sababu alitumia miguu yote miwili, kosa kubwa kuliko hata lile lililosababisha nahodha wa Man.City kuonyeshwa kadi nyekundu wakati wa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United siku ya jumapili.

Lakini Gerrard hakukubaliana na Mancini na kumjibu kwa hamaki.

Gerrard alimwendea Mancini wakati kocha huyo akisubiri kuzungumza na wandishi wa habari.

Nahodha huyo wa Liverpool alimnyooshea kidole Mancini na kumuambia wewe unadai kua Wayne Rooney alijitahidi na kufanikiwa kumuondoa Kompany kwa kadi nyekundu na leo wewe unatumia ujanja ule ule ukitaka Johnson aonyeshwe kadi nyekundu.

Alimsikiliza na kumjibu, nina uhuru wa kusema nitakalo. Mengine aliyoyasema hayakueleweka kutokana na lugha.

Hapa Gerrard alitikisa kichwa na kugeuka na kuondoka lakini alimuacha Mtaliano akichemka na kuwambia wandishi wa habari kua Gerrard amenihamakia.

Mbali na matukio yaliyofuatia kipigo cha Manchester City, ushindi wa Liverpool ni nyota njema ya kuweza kushiriki fainali ya kwanza tangu mwaka 1996 baada ya duru ya kwanza ya nusu fainali ya kombe la Carling.

Bao la Liverpool lilipatikana kupitia mkwaju wa peneti na kufungwa na nahodha Steven Gerrad baada ya Daniel Agger kufanyiwa madhambi na Stefan Savic ndani ya eneo la hatari.

City sasa inakabiliwa na kigezo kikubwa cha kwanza tangu mwezi Febuari mwaka 2008 ingawa bado kuna uwezekano wa kuinyuka Liverpool katika mechi ya marudiano wiki mbili zijazo kwenye uwanja wa Liverpool wa Anfield.