Arsenal yalala, Newcastle yaibuka

Matumaini ya Arsenal kusogelea nafasi nne bora za juu za Ligi ya kandanda ya England yalivurugwa na Swansea waliosakata kandanda murua na kuweza kupata pointi tatu muhimu kwa kuilaza Arsenal mabao 3-2 katika mchezo uliokuwa wa kusisimua.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Robin Van Persie aliifungia Arsenal bao la kwanza

Arsenal walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya nne kwa bao la Robin van Persie, lakini wageni hao walionekana kuzidiwa katika kila idara na vijana wa Swansea.

Scott Sinclair aliisawazishia Swansea kwa mkwaju wa penalti baada ya Aaron Ramsey kumkwatua Nathan Dyer ndani ya eneo la hatari.

Nathan Dyrea aliipatia Swanse bao la pili katika kipindi cha pili kwa makosa ya walinzi wa kati wa Arsenal

Theo Walcott aliisawazishia Arsenal kwa bao la pili na dakika moja baadae Danny Graham akaipatia Swansea bao la tatu la ushindi.

Na bao maridadi lililofungwa na Leon Best katika kipindi cha kwanza liliinua Newcastle hadi nafasi ya sita ya msimamo wa Ligi Kuu ya England na kumvurugia meneja mpya wa QPR Mark Hughes mechi yake ya kwanza.

QPR mara mbili mikwaju yao iligonga mwamba katika kipindi cha kwanza kwa michomo ya Shaun Wright-Phillips na Jay Bothroyd.

Lakini Newcastle walizinduka kutoka usingizini mwanzoni mwa kipindi cha kwanza na Best alifunga bao maridadi baada ya kuwazunguka walinzi wa QPR.

Bothroyd alipoteza nafasi mbili nzuri kuipatia QPR mabao katika kipindi cha pili lakini walinzi wa Newcastle walionekana kukaa imara.