Chelsea yakamilisha usajili wa Cahill

Klabu ya Chelsea imekamilisha mipango ya kumsajili Gary Cahill kutoka klabu ya Bolton Wanderers kwa gharama ya paundi zinazofika milioni 7.

Image caption Gary Cahill tayari ajiunga na Chelsea akitokea Bolton

Cahill, mwenye umri wa miaka 26, alifaulu vipimo vya afya yake siku ya Jumamosi, kabla ya kuhudhuria mechi ambapo Chelsea ilishinda bao 1-0 dhidi ya Sunderland katika uwanja wa Stamford Bridge.

"Chelsea ni klabu kubwa ambayo ina malengo ya kushinda vikombe," alisema mlinzi huyo anayechezea pia timu ya taifa ya England.

"Ni nafasi kubwa kwangu kuwa miongoni mwa mafaniko hayo. Nafasi kama hii kamwe huwezi kuiachilia," aliongeza.

Chelsea na Bolton walikubaliana gharama za uhamisho mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas amebainisha klabu na mchezaji huyo walikuwa wakitafuta muafaka wa kukubaliana kiwango cha mshahara.

Kuna taarifa nyingine zilikuwa zikisema Manchester United pia walikuwa wakimyatia Cahill, ambaye mkataba wake unamalizika na timu ya Bolton mwishoni mwa msimu huu.

Lakini Villas-Boas hatimaye amekamilisha mkataba huo na kuimarisha safu yake ya ulinzi wakati huu wa patashika za Ligi Kuu, Ubingwa wa Ulaya na kombe la FA.

Mlinzi mwengine wa kati wa Chelsea Alex anajiandaa kuondoka katika klabu hiyo na Chelsea imekwishafanya mazungumzo na klabu ya magharibi mwa London ya QPR.