Man U nje FA

Mkwaju wa dakika za mwishomwisho wa Dirk Kuyt uliiwezesha Liverpool siku ya Jumamosi kuiondoa Manchester United katika mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA, ilipoishinda magoli 2-1.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mashabiki wa Liverpool walimzomea Evra mara kwa mara

Bao la mshambulizi huyo lilikuwa muhimu sana katika mechi iliyochezewa uwanja wa nyumbani wa Liverpool wa Anfield.

Awali ilielekea kana kwamba timu hizo zitakutana tena katika uwanja wa Old Trafford, kwani Ji-Sung Park alikuwa amefanikiwa kuisawazishia Manchester United.

Nyota ya Liverpool inaelekea kung'ara, kwani meneja Kenny Dalglish tayari amekiwezesha klabu kufanikiwa kuingia fainali ya Kombe la Carling, mechi ambayo itakuwa ni nafasi yao ya kwanza tangu mwaka 1996 kucheza katika uwanja wa Wembley, baada ya kuiondoa Manchester City.

Mechi hiyo ilichezwa kukiwa na wasiwasi kwamba ilikuwa ni rahisi ghasia kuanza, kufuatia mchezaji wa Liverpool, Luis Suarez, hivi majuzi kuchukuliwa hatua kwa kutumia matamshi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya nahodha wa Manchester United, Patrice Evra.

Suarez, kutoka Uruguay, pia aliadhibiwa na chama cha soka cha FA asicheze katika mechi nane.

Licha ya makocha wa timu zote kuwataka mashabiki kuwa watulivu, Evra alizomewa mara kwa mara katika mechi hiyo.