Gabon yaongoza kundi C

Gabon Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wachezaji wa Gabon wameandikisha ushindi wao wa tatu mfululizo

Gabon, ambayo inashirikiana na Equatorial Guinea kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu, Jumanne ilifanikiwa kuongoza kundi la C, baada ya kuishinda Tunisia 1-0 katika mechi iliyochezewa mjini Franceville.

Lilikuwa ni bao la tatu kwa Pierre-Emerick Aubameyang katika mashindano hayo, kufuatia kuandaliwa vyema mpira na nahodha wake, Daniel Cousin.

Kwa taratibu aliuelekeza mpira langoni, huku miguu ya kipa wa Tunisia, Rami Jeridi, ikimsaidia katika kuusindikiza mpira wavuni.

Mchezo wa Tunisia haukuwa burudani ya kuvutia, lakini licha ya hayo, timu hiyo imemaliza hatua ya makundi ikiwa katika nafasi ya pili, nyuma ya timu ya Panthers ya Gabon.

Timu zote zilianza mechi zikiwa tayari zimefuzu kwa robo fainali, lakini Gabon ilitaka angalau itoke sare katika mechi hiyo, ili kujihakikishia kwamba itacheza mechi yake ya robo fainali ikiwa nyumbani, mji mkuu wa Libreville.

Kwa upande wa Morocco, angalau ilijitoa aibu katika mechi nyingine ya kundi C, wakati ilipoishinda Niger 1-0.

Younes Belhanda alitia mpira wavuni, zikiwa zimesalia dakika 11 tu kabla ya mechi kumalizika, mchezo ambao ilielekea haukuwavutia mashabiki wengi.

Timu zote ziliingia uwanjani zikiwa na matumaini ya kujipatia pointi zake za kwanza katika mashindano ya mwaka huu, baada ya kulemewa katika mechi zao zote za awali.

Lakini Niger inabidi kurudi nyumbani, baada ya kushiriki katika mashindano yao ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika, wakishindwa katika mechi zote.

Jumatano kunatazamiwa kuwa na burudani ya kutosha, kwani mechi za mwisho za makundi zitachezwa.

Hizi ni mechi za kundi D, wakati timu za Ghana, Guinea na Mali zitakuwa na kibarua kigumu kujitahidi katika kuwania nafasi mbili za robo fainali zilizosalia, na Botswana inatazamiwa kujipatia ushindi katika angalau mechi yake ya mwisho katika hali ya kujiandaa kuelekea nyumbani.