Fabio Capello ajiuzulu

Fabio Capello Haki miliki ya picha PA
Image caption Utata kuhusiana na suala la John Terry umemfanya kujiuzulu

Fabio Capello amejiuzulu kama meneja wa timu ya taifa ya soka ya England, chama cha FA kimethibitisha habari hizo.

Capello amejiuzulu baada ya kukutana na mwenyekiti wa chama cha FA cha England, David Bernstein, na katibu mkuu Alex Horne, katika afisi za uwanja wa Wembley.

Taarifa ya FA ilielezea: "Chama cha soka cha FA kinathibitisha kwamba Fabio Capello leo amejiuzulu kama meneja wa timu ya England."

Siku ya Jumatatu, Capello, ambaye ni raia wa Italia, katika magazeti ya Italia alielezea kutopendezwa na hatua ya chama cha FA kumvua John Terry unahodha wa timu ya taifa ya England.

Taarifa ya FA iliendelea kueleza; "Katika mkutano ulioendelea kwa zaidi ya saa nzima, hatua ya Fabio kujiuzulu ilikubaliwa, na ataacha madaraka hayo mara moja".

Bernstein alielezea: "Ningelipenda kusisitiza kwamba wakati wa mkutano, na katika wakati wote ambao Fabio amekuwa meneja wa timu ya taifa, tabia yake imekuwa ni ya mtu aliyesimamia kazi yake kwa heshima".

Mkutano wa Bernstein akiwa na maafisa wakuu wa timu ya England, kukutana na waandishi wa habari, unatazamiwa kufanyika Alhamisi, saa sita mchana za Uingereza, katika uwanja wa Wembley.

Chama cha FA kimeelezea hakitatoa maelezo zaidi hadi baada ya mkutano huo.

John Terry, mchezaji wa Chelsea, na mwenye umri wa miaka 31, inadaiwa alitumia matamshi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya mchezaji wa QPR, Antonio Ferdinand.

Terry anakanusha madai hayo, na kesi yake itasikilizwa mwezi Julai.

Siku ya Jumapili, Capello akizungumza katika kituo cha matangazo cha RAI nchini Italia, alisema haamini uongozi wa michezo unafaa kumuadhibu mtu, huku akisubiri uamuzi kutolewa na mahakama.